Uamuzi wa Mahakama Kenya wamuacha Gachagua njiapanda
9 Juni 2026
Aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, anatarajiwa kuelekea katika Mahakama ya Rufaa baada ya Mahakama Kuu kuidhinisha kuondolewa kwake madarakani. Uamuzi huo umetoa pigo kubwa kwa juhudi zake za kisiasa huku ukifungua sura mpya ya mvutano wa kisheria unaomhusu.
Katika uamuzi uliotolewa usiku wa kuamkia leo, jopo la majaji watatu lilikataa hoja nyingi zilizowasilishwa na Gachagua. Hata hivyo, mahakama ilisema baadhi ya haki zake za kikatiba zilikiukwa na kuamuru alipwe fidia ya shilingi milioni 50 na Seneti.
Uamuzi huo unamaanisha kuwa kuondolewa kwake madarakani kunabaki halali. Pia unafungua njia kwa Kithure Kindiki kuendelea kuhudumu kama Naibu Rais wa Kenya.
Wakili wa Gachagua, Ndegwa Njiru, ameukosoa uamuzi huo akisema mahakama ilikubali kuwa haki za mteja wake zilikiukwa lakini ikashindwa kutoa suluhisho stahiki. Amesema timu yake ya wanasheria itatafuta haki katika ngazi ya juu zaidi ya mahakama.
Je, Gachagua bado ana nafasi kisiasa?
Licha ya kushindwa mahakamani, wachambuzi wanaamini Gachagua bado anaweza kutumia uamuzi huo kuimarisha simulizi yake kwamba amekuwa akilengwa kisiasa. Kwa muda mrefu amekuwa akijitambulisha kama mwathirika wa njama za kisiasa zinazolenga kumzuia kushiriki kikamilifu katika siasa za Kenya.
Mtaalamu wa masuala ya uongozi Likaka Lichetu anasema Gachagua bado ana ushawishi mkubwa katika eneo la Mlima Kenya. Kwa mujibu wake, msingi wake wa kisiasa haujatoweka na unaweza kuendelea kuwa nguzo muhimu ya upinzani kuelekea uchaguzi wa mwaka 2027.
Hata hivyo, wachambuzi wengine wanaonya kuwa uamuzi huo unaweza kuathiri hadhi yake ya kisiasa kwa muda mrefu. Maswali kuhusu uhalali wake wa kugombea nafasi za uchaguzi yanaweza kuendelea kujitokeza hadi pale mahakama za juu zitakapotoa mwelekeo wa mwisho.
Macho yaelekezwa Mahakama ya Rufaa
Sasa matumaini ya Gachagua yako katika Mahakama ya Rufaa, ambayo itapitia upya hoja za kisheria zilizowasilishwa dhidi ya mchakato wa kumuondoa madarakani. Uamuzi huo unaweza kuwa wa mwisho katika kuamua mustakabali wake wa kisiasa.
Likaka Lichetu anaamini kuna uwezekano mkubwa mahakama za juu pia zikaafikiana na hitimisho kwamba mchakato wa kumuondoa madarakani ulifanyika kwa mujibu wa sheria. Hata hivyo, anasema kesi hiyo bado ina umuhimu mkubwa wa kisiasa na kikatiba.
Baada ya kuondolewa madarakani, Gachagua alianzisha chama cha DCP na kuanza kampeni za kujiimarisha kisiasa hasa katika eneo la Mlima Kenya. Wafuasi wake wanamuona kama mrithi wa kisiasa wa eneo hilo baada ya kuondoka madarakani kwa Uhuru Kenyatta.
Kwa sasa, vita vya kisheria vinaendelea huku vita vya kisiasa vikichukua mkondo mpya. Mahakama ya Rufaa sasa ndiyo inayotarajiwa kutoa mwelekeo kuhusu hatua inayofuata katika safari ya kisiasa ya Rigathi Gachagua.