1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gachagua augua ghafla katikati mwa kesi yake mbele ya Seneti

17 Oktoba 2024

Kesi ya kumuondoa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, iliingia katika hali ya sintofahamu Alhamisi baada ya wakili wake kusema kuwa Gachagua ameugua na kulazwa hospitalini.

Kenya | Mkutano wa habari wa Naibu wa Rais wa Kenya Rigathi Gachagua
Wakili wa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua amesema mteja wake anaumwa sana na amepelekwa hospitalini.Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Taarifa hiyo ilisababisha Spika wa Seneti, Amason Kingi, kuahirisha vikao hadi saa 11 jioni, jambo ambalo linazidi kuongeza msisimko kwenye mzozo wa kisiasa uliokuwa ukifuatiliwa sana katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

"Ukweli wa kusikitisha ni kwamba Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya anaumwa sana, na... yuko hospitalini," alisema wakili Paul Muite mbele ya baraza hilo la juu la Bunge la Kenya, akieleza kutokuwepo kwa Gachagua.

Licha ya hali hiyo, Kingi alibainisha kuwa Gachagua alitarajiwa kutoa ushahidi saa 11 jioni, akisema, "Hii ni kesi yenye muda maalum, kwa bahati mbaya. Imetolewa agizo hivyo."

Seneti ilikuwa inatarajiwa kutoa uamuzi wake Alhamisi jioni baada ya siku ya pili ya kusikiliza hoja za pande mbili kabla ya kuamua kumuondoa madarakani Naibu Rais, nafasi ya pili kwa Rais William Ruto.

Soma pia: Seneti ya Kenya kupiga kura kuamua hatma ya Gachagua

Kesi hii ilifuatia kura ya kihistoria iliyopigwa wiki iliyopita katika Bunge la Taifa ya kumwondoa Gachagua kwa mashtaka 11, yakiwemo ufisadi, kutotii mamlaka, kudhoofisha serikali, na kuchochea siasa za kikabila.

Kesi hiyo iliendelea baada ya Gachagua, maarufu kama "Riggy G", kushindwa katika majaribio kadhaa ya korti kuzuia mchakato huo.

Gachagua amekanusha mashtaka yote, na hadi sasa hakuna kesi ya jinai iliyofunguliwa dhidi yake, lakini atatolewa ofisini moja kwa moja ikiwa Seneti itaidhinisha kuondolewa kwake.

Kikao cha Baraza la Seneti kikisikiliza hoja za kuunga mkono na kupinga kutimuliwa kwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua. Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Iwapo hili litafanyika, Gachagua atakuwa Naibu Rais wa kwanza kuondolewa madarakani kwa njia hii tangu utaratibu wa kufukuzwa ofisini ulipowekwa kwenye Katiba mpya ya Kenya ya mwaka 2010.

Hata hivyo, Gachagua anaweza kupinga kuondolewa kwake mahakamani baada ya mchakato wa bunge kukamilika.

Majina ya wanaoweza kurithi nafasi ya Gachagua yatajwa

Miongoni mwa majina yanayopigiwa upatu kuchukua nafasi ya Gachagua ni Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki, Waziri wa Mambo ya Nje na Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri Musalia Mudavadi, na Gavana wa Kaunti ya Kirinyaga, Anne Waiguru.

Fursa ya Gachagua kuendelea kuzuia mchakato wa kumwondoa ni ndogo ikiwa wabunge wa upinzani kwenye Seneti yenye viti 67 wataunga mkono chama tawala, kama ilivyoshuhudiwa kwenye kura ya Bunge la Taifa tarehe 9 Oktoba.

Tofauti na mchakato wa Bunge la Taifa, ambapo wabunge walipiga kura kwa hoja nzima, maseneta wanahitaji kuunga mkono tu shtaka moja kwa theluthi mbili ya kura ili kuondolewa kwa Gachagua kufanikiwe.

Soma pia: Mahakama Kenya yakataa kuzuia kura ya seneti kuhusu kumng'oa madarakani naibu wa rais

Gachagua, mfanyabiashara maarufu kutoka kabila kubwa la Kikuyu nchini Kenya, alipambana na kashfa za ufisadi hapo awali na kuwa Naibu Rais baada ya kushirikiana na Ruto katika uchaguzi wa mwaka 2022.

Hata hivyo, wiki za karibuni amekuwa akilalamika kuwa amesalitiwa na kupuuzwa na rais, huku akidaiwa kuunga mkono maandamano yanayoongozwa na vijana dhidi ya serikali yaliyotokea mwezi Juni.

Spika wa Seneti Amasoni Kingi aliahirisha kikao hadi saa 11 jioni na kumtaka Naibu wa Rais awepo kujitetea. Picha: Tony Karumba/AFP/Getty Images

Mvutano wa kisiasa umeongezeka tangu maandamano hayo, yaliyoibuka kutokana na ongezeko la ushuru, na kufichua migawanyiko katika ngazi za juu za serikali.

Gachagua akana mashtaka, ataka amani 

Kabla ya kura ya wiki iliyopita, Gachagua alikanusha vikali mashtaka dhidi yake akiyaita "madai ya upuuzi" na kusema jitihada za kumwondoa zinapuuza matakwa ya wananchi waliochagua serikali ya mwaka 2022.

Alipohutubia waumini katika ngome yake ya kisiasa ya eneo la Kati mwa Kenya Jumapili iliyopita, aliwataka wafuasi wake kubaki watulivu, akisema, "Tuendelee kuhubiri na kudumisha amani bila kujali matokeo.

Soma pia: Bunge la Kenya lapiga kura kumuondoa madarakani Gachagua

Kenya ni nchi yetu." Wakili wake alidai kuwa mchakato wa kumwondoa ulikuwa wa haraka na usio wa haki, lakini Mahakama Kuu iliamua Jumatano kuwa mchakato huo unaweza kuendelea, hivyo kufungua njia kwa vikao vya Seneti.

Rais Ruto hajatoa kauli yoyote ya wazi kuhusu mchakato huu wa kumwondoa Gachagua, ingawa Gachagua alisema kuwa mchakato huo haungeendelea bila baraka za mkuu wake.