Gaddafi aanza kupoteza udhibiti wa nchi
23 Februari 2011Waandamanaji wanaonekana kuwa na udhibiti kamili kwenye mji wa pwani ya mashariki wa Tobruk, na kuna taarifa pia kwamba miji ya magharibi ya Libya nayo imeanza kutoka mikononi mwa Muammar Gaddafi.
Udhibiti huu wa waandamanaji unajumuiya eneo zima la mpakani mwa Libya na Misri, kuanzia mji wa Tobruk, Benghazi, ambao ni wa pili kwa ukubwa baada ya Tripoli hadi Ajdabiya ulio magharibi kabisa mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, wanajeshi wa Gaddafi katika maeneo hayo aidha wamejiunga na waandamanaji au wamejitenga kando.
Wakaazi wa mji mwengine wa Bayda, wameiambia AFP kuwa, wapiganaji wanaomuunga mkono Gaddafi walikamatwa na kuuawa na waandamanaji.
Hata hivyo, serikali ya Libya imeendelea kuchukua hatua za kile alichokiita jana Gaddafi kwenye hotuba yake kwa taifa, kama "kudhibiti uasi" dhidi ya Jamhuri ya Kiarabu ya Libya.
Takwimu za karibuni kabisa zinakisia kuwa tayari watu 1000 wameshapoteza maisha tangu vikosi vya Gaddafi na mamluki wa kigeni kuanza kuwashambulia waandamanaji.
Wakati huo huo, jumuiya ya kimataifa imeendelea kumgeuka na kumuonya Gaddafi. Rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkouzy, ameutaka Umoja wa Ulaya uiwekee vikwazo vya biashara Libya, huku Rais wa Iran, Mahmoud Ahmedinejad, akilaani vikali hatua ya serikali ya Libya kuwashambulia raia wake.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Hispania, Trinidad Jimenez, amesema leo hii kuwa, Gaddafi tayari ameshapoteza uhalali wa kuiongoza Libya.
"Kiongozi wa kisiasa aliyeamua kuwapiga mabomu raia wake mwenyewe, huwa ameshapoteza uhalali wa kuendelea kuongoza nchi yake." Amesema Bi Jimenez.
Katika hatua nyengine, ubalozi wa Libya nchini Austria, umetangaza kulaani mashambulizi ya serikali yao dhidi ya waandamanaji. Huu ni utakuwa ni ubalozi wa nane wa Libya kujitenga na matendo ya serikali yao, tangu serikali hiyo ianze kukabiliana na waandamanaji siku nne zilizopita.
Ofisi za ubalozi wa nchi hiyo nchini Indonesia, Malaysia, India, Uingereza na Marekani, ni miongoni mwa balozi ambazo hazikubaliani na matendo ya Gaddafi dhidi ya waandamanaji.
Wakati hali ikitoka kubaya ikielekea kubaya zaidi, Uingereza, Marekani na Romania zimekuwa nchi za hivi karibuni kabisa, kutangaza mipango yao ya kuwaondosha watu wao.
Tayari nchi za Uturuki, Urusi, Tunisia na Misri zimeshaanza kuwaondoa raia wao, huku India ikikamilisha mpango wa uokozi kwa raia wake wakaribiao 20,000, ambao wamekuwa wakifanya kazi nchini Libya.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman