Gambia yaunda jopo kuchunguza jaribio la mapinduzi
28 Desemba 2022Msemaji wa serikali ya Gambia Ebrima Sankareh amesema jopo hilo linawahusisha watumishi kutoka taasisi za serikali ikiwemo wizara ya sheria, ofisi ya usalama wa taifa, vikosi vya jeshi, polisi na idara ya ujasusi waliapishwa hapo jana Jumanne.
Gambia ilisema Jumatano wiki iliopita ilizuia jaribio la mapinduzi na kuwashikilia baadhi ya wanajeshi, ikiwa ni pamoja na kapteni na luteni pamoja na wanajeshi wengine 5 ili kusaidia uchunguzi wa madai hayo huku wengine wawili wakitafutwa.
Mwanasiasa wa upinzani Momodou Sabally, waziri wa zamani wa masuala ya Rais chini ya kiongozi wa zamani Yahya Jammeh, pia anashikiliwa baada ya kuonekana kwenye video akisema rais wa sasa angepinduliwa kabla ya uchaguzi ujao wa mashinani.
Afrika Magharibi imetikiswa na mkururo wa mapinduzi ya kijeshi tangu mwaka 2020.