Gauck aupigia debe Umoja wa Ulaya
5 Februari 2015Akizungumza na wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Alhamisi (05.04.2015) mjini Arusha kaskazini mwa Tanzania Rais Gauck amesema Umoja wa Ulaya umeonyesha nia ya kufikia maridhiano na kwamba hata katika nyakati ngumu imeendelea kushikilia kile wanachokiamini kwa pamoja.Kauli hiyo ya Gauck inakuja wakati kukiwa na mjadala juu ya mustakbali wa Ugiriki katika Umoja wa Ulaya.
Bila ya kutaka kuuingilia moja kwa moja mjadala unaoendelea kuhusu Waziri Mkuu mpya wa Ugiriki Alexis Tsipras rais huyo wa Ujerumani ameongeza kusema kwamba maadili hayo ya Umoja wa Ulaya ni muhimu katika kufikia maridhiano au venginevyo kuwa na subira na ikibidi kuweka kando japo kidogo maslahi ya nchi.
Gauck ameipigia debe sera hiyo ya Umoja wa Ulaya licha ya kukabiliwa na matatizo kwa wabunge wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki za Tanzania, Kenya,Uganda,Burundi na Rwanda ambazo zinataka kuwa na ushirikiano wa karibu wa kisiasa na uchumi sawa na ule ulioko katika Umoja wa Ulaya.
Msisikilize wachochezi wasioitakia mema Ulaya
Rais huyo wa Ujerumani amesema licha ya kuwepo kwa serikali mpya ya sera kali za mrengo wa shoto nchini Ugiriki ambapo watu wamekuwa wakiona kama vile kuna kitu kibaya kitatokea huko mbele kwa kutangaza mara kwa mara kwamba Umoja wa Ulaya utavunjika na sarafu ya euro haitotumika. Gauck ametaka watu wawasiwaamini wale wanaofanya propaganda hizo za kuanguka kwa Umoja wa Ulaya.Amesema hadi sasa imethibitika kwamba hawako sahihi.
Kiongozi huyo wa Ujerumani ameongeza kusema kwamba umoja huo wa mataifa ya Ulaya bado ni mkubwa kuliko vile ilivyokuwa kabla una mshikamano wa kusaidiana wakati nchi mwanachama inapohitaji msaada na iko tayari kuwa na mazungumzo yao wenyewe yenye tija.
Amesema kutokana na ugaidi wa wanamgambo wa itikali kali wa Kiislamu dhidi ya kijarida cha dhihaka cha Ufaransa cha "Charlie Hebdoo" kumeifanya Ulaya kuwa kitu kimoja katika kuenzi maadili yao ya pamoja.Hatua ya Urusi kuvunja sheria ya kimataifa katika suala la Ukraine anasema pia hivi karibuni imezidi kuzikurubisha pamoja nchi wanachama wa umoja huo.
Vita dhidi ya ujangili
Katika ziara yake hiyo ya Arusha Gauck awali alikuwa amepangiwa kukutana na Rais wa Mahakama ya Haki za Binaadamu ya Afrika jaji mwandamizi wa zamani wa Tanzania Augustine Ramadhani.
Mchana huu anatembelea Mbuga ya Taifa ya Serengeti kama sehemu ya ziara yake rasmi nchini Tanzania pamoja na kuzinduwa kituo cha kupambana na ujangili kilichojengwa na Shirika la Bustani ya Wanyama ya Frankfurt (FZS). Mkurugenzi wa shirika hilo Christof Schenk ameonya kwamba ujangili wa tembo na vifaru unatishia utengamano wa mataifa ya Afrika na kwamba fedha nyingi zinazopatikana katika mauaji haramu ya wanyama hao zinachochea rushwa katika mataifa hayo.
Amesema ujangili huleta rushwa kama vile ilivyo kwa biashara ya madawa ya kulevya.Inakadiriwa tembo 30,000 huuwawa kila mwaka ikiwa ni pamoja na wale wengi wanaouwawa nchini Tanzania.
Mwandishi : Mohamed Dahman/dpa/AP
Mhariri : Josephat Charo