1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gavana wa Beki Kuu atimuliwa Nigeria

21 Februari 2014

Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria amemsimamisha kazi gavana wa Benki Kuu Sanusi Lamido ambaye amekuwa mkosaji mkubwa wa serikali kwa kutochukuwa hatua za kupambana na rushwa.

Sanusi Lamido Sanusi Gavana wa Benki Kuu ya Nigeria.
Sanusi Lamido Sanusi Gavana wa Benki Kuu ya Nigeria.Picha: Reuters

Kwa mujibu wa agizo la rais lililotolewa jana Sarah Alade naibu gavana ameteuliwa kushika nafasi yake.Msemaji wa rais Reuben Abati amesema Sanusi ameshindwa kufuata taratibu za matumizi ya fedha katika kusimamia bajeti ya Benki Kuu na ametumia fedha kinyume na sheria kwenye miradi ilioko nje ya mamlaka yake.

Sanusi mwenye umri wa miaka 52 mara kwa mara amekuwa akiishutumu serikali kwa kutochukuwa hatua za kupambana na rushwa.Miongoni mwa mambo mengine ameishutumu kampuni ya mafuta ya taifa NNPC kwa kufanya ubadhirifu wa dola bilioni 20. Sanusi ni mmojawapo wa watu muhimu katika harakati za kupiga vita rushwa nchini Nigeria ambayo imetopea katika taifa hilo lenye kuzalisha mafuta kwa wingi barani Afrika na lenye idadi kubwa kabisa ya watu barani humo.

Mashirika yasio ya kiserikali yenye kupambana na rushwa na wanasiasa wa upinzani wanaona kutimuliwa kwa gavana huyo ni kurudi nyuma kwa katika juhudi zao za kupigania kuwepo uwazi na utawala wa sheria nchini Nigeria.

Kudhoofisha vita dhidi ya rushwa

Auwala Ibrahim Musa Mwenyekiti wa Muungano wa Zero Corruption nchini Nigeria ambao ni mshirika wa Shirika la Kimataifa la kupiga vita rushwa Transparency International amekaririwa akisema " Kwa kweli hatua hiyo inazidisha na kuongeza rushwa nchini kwa sababu pia inawavunja moyo watu kusema ukweli na kufichuwa rushwa.Iwapo gavana wa Benki Kuu anaweza kuonewa hiyo inamaanisha kwamba hakuna mtu aliye salama."

Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria.Picha: Pius Utomi ekpei/AFP/Getty Images

Musa anaona kwamba kusitishwa kwa gavana huyo kumechochewa kisiasa na kwamba rais amemtimuwa kwenye wadhifa huo kabla ya muda wake kumalizika hapo mwezi wa Juni ili asifichuwe zaidi maovu ya nchi hiyo.Katika mahojiano na DW Musa amelaani kusitishwa kwa gavana huyo kutokana na kile alichosema kuwa Rais amepindukia madaraka yake kwa kuwa katiba haimpi haki hiyo ya kumtimuwa gavana wa Benki Kuu na kwamba ni bunge la taifa ndio lenye mamlaka hayo.

Ishara mbaya

Sanusi mwenyewe anataka kupinga kutimuliwa kwake huko mahakamani lakini hakusudii kurudishwa kwenye wadhifa huo bali anataka kuyakinisha iwapo rais ana haki ya kumtimuwa gavana wa benki kuu.

Benki Kuu ya Nigeria ilioko katika mji mkuu wa nchi hiyo Abuja.Picha: public domain

Buba Galadima wa chama cha upinzani nchini Nigeria cha All Progressive Congress (APC) anaona kutimuliwa kwa gavana huyo kwenye wadhifa wake kunatokona na kile alichokifichua. anasema lazima inahusiana na madai yake kwamba kulikuwa hakuna matumizi ya malipo ya zaidi ya dola bilioni 49 fedha za walipakodi wa Nigeria zilizotokana na mauzo ya mafuta ghafi.Na amesisitiza kwamba zichunguzwe ambapo imebainika kwamba dola bilioni 20 zilikuwa zimeibwa na vigogo visivyoguswa serikalini.

Amesema alikuwa akifikiria kwamba serikali ya Nigeria ingelimpa Sanusi medali na sio kumsimamisha kazi au kumundowa. Ni ishara mbaya katika mapambano ya kupiga vita rushwa nchini Nigeria wachumi pia wana hofu kwamba kushamiri tena kwa rushwa pia kunaweza kuathiri uwekezaji katika uchumi wa Nigeria.Benki kuu ya Nigeria hapo jana ilisitisha kwa muda biashara ya kubadilisha fedha za kigeni na katika masoko ya hisa.Thamani ya sarafu ya Nigeria Naira pia ilishuka sana hapo jana kabla ya serikali kuchukuwa hatua za kuirudishia thamani.

Mwandishi: Mohammed Dahman/Steffen,Sarah

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman