1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gavana: Watu wanakimbia operesheni ya Israel mji wa Jenin

23 Januari 2025

Afisa mmoja wa Kipalestina amesema leo Alhamisi kwamba mamia ya watu wameanza kuzikimbia nyumba zao kwenye mji wa Jenin ulioko Ukingo wa Magharibi ambako vikosi vya Israel vinafanya operesheni kubwa ya kijeshi.

Uvamizi wa jeshi la Israel huko Jenin
Mvulana wa Kipalestina akinyoosha mkono hewani wakati wanajeshi wa Israel wakielekea kukagua alichokibeba wakati wa uvamizi wa Israel kwenye wa Jenin eneo la Ukingo wa Magharibi. Picha: Ronaldo Schemidt/AFP

Gavana wa mji wa Jenin, ulio kitovu cha operesheni ya kijeshi ya Israel, Kamal Abu al-Rub, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba mamia ya wakaazi wa kambi ya wakimbizi ya mji huo wameanza kuondoka baada ya kuamriwa na vikosi vya Israel.

Amesema amri ya kuwataka kuondoka imetolewa kupitia vipaza sauti vilivyofungwa kwenye droni na magari ya kijeshi. Jeshi la Israel lenyewe limekanusha taarifa hizo likisema halina taarifa yoyote juu ya amri ya kuwataka wakaazi wa Jenin kuondoka.

Hata hivyo wakaazi kadhaa waliozungumza na AFP wamesema wameshuhudia wenzao kadhaa wakikusanya virago na kuondoka.

Mkaazi mmoja aliyetambulishwa kwa  majina ya Salim Saadi amesema wanajeshi wa Israel wako mbele ya nyumba yake na wangeweza kuingia wakati wowote.

Mikanda ya video iliyotolewa na AFP imeonesha pia watu wakiukimbia mji wa Jenin kwa mguu tangu jana Jumatano huku sauti za droni za jeshi la Israel zikisikika juu ya anga la mji huo

Israel yasema kampeni yake ya kijeshi inalenga kudhibiti ugaidi

Israel ilifanya uvamizi kwenye mji wa Jenin kuanzia siku ya Jumanne na hadi sasa vikosi vyake vimewakamata Wapalestina kadhaa.

Mpiga picha wa AFP ameshuhudia msusuru wa wanaume waliovalishwa sare za mahabusu huku wakiwa wamefungwa vitambaa machoni wakisafirishwa kutoka Ukingo wa Magharibi.

Uvamizi wa Israel huko Jenin, Ukingo wa Magharibi.Picha: Mohammed Turabi/IMAGESLIVE/ZUMA Press Wire/picture alliance

Waziri Mkuu wa Israel amesema lengo la oparesheni hiyo iliyopachikwa jina la "Ukuta wa Chuma" ni kutokomeza ugaidi kwenye eneo hilo. Amesema kampeni hiyo ya kijeshi ni sehemu ya mkakati mpana wa kuishinda nguvu Iran katika kila eneo inakopeleka silaha iwe "Ukanda wa Gaza, Lebanon, Syria, Yemen" na hata Ukingo wa Magharibi.

Utawala mjini Tel Aviv unaituhumu Iran inayoyaunga mkono makundi kadhaa ya wapiganaji kwenye  kanda ya Mashariki ya Kati kuwa sasa inajaribu kufadhili wanamgambo eneo la Ukingo wa Magharibi.

Mapema hii leo ripoti ziliarifu kwamba tangu uvamizi huo ulipoanza Wapalestina wasiopungua 12 wameuawa na wengine zaidi ya 40 wamejeruhiwa.

Gavana wa mji wa Jenin alizungumzia pia uharibifu uliofanywa na jeshi la Israel kwenye miundombinu ya mji huo ikiwemo matingatinga yake kuchimbua barabara zinazoelekea kwenye kambi kubwa ya wakimbizi na hospitali muhimu ya serikali.

Wakaazi waliokimbia kaskazini mwa Gaza wajiandaa kurejea eneo hilo

Uharibifu uliofanywa huko kaskazini mwa Gaza baada ya miezi 15 ya vita. Picha: Omar Al-Qattaa/AFP/Getty Images

Huko kwenye eneo lingine la Wapalestina la Ukanda wa Gaza, wakaazi wake wanajitayarisha kurejea kaskazini mwa ukanda huo ulioharibiwa kwa vita ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyotiwa saini na kuanza kutekelezwa Jumapili iliyopita.

Inaarifiwa wale waliobakia kwenye eneo hilo wanajiandaa kupokea makundi makubwa ya watu yaliokimbilia kusini mwa Gaza chini ya amri za jeshi la Israel iliyotolewa wakati wa kampeni yake kubwa ya kupambana na kundi la Hamas.

Picha zimeonesha wanaume wakitayarisha mahema kuzingojea familia zao ambazo zitarejea kwenye eneo ambalo kwa sehemu kubwa limeharibiwa na mfululizo wa makombora ya jeshi la Israel katika kipindi cha miezi 15 ya vita.

Inaaminika wengine watafanya safari ya kurejea kaskazini mwa Gaza kuanzia Jumamosi pale Hamas itakapowaachia huru mateka wengine wa Israel inaowashikilia.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW