1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dozi milioni 10 za Chanjo dhidi ya Malaria zimetolewa Afrika

Angela Mdungu
23 Januari 2025

Shirika la Kimataifa linaloshughulika na kuboresha upatikanaji wa chanjo la Gavi limesema karibu dozi milioni 10 za Malaria zilipelekwa Afrika katika mwaka wa kwanza wa utoaji chanjo kote barani humo.

Mapambano dhidi ya Malaria Afrika
Chanjo dhidi ya Malaria zimeendelea kutolewa AfrikaPicha: Desire Danga Essigue/REUTERS

Hatua hiyo imepigwa ikiwa ni katika juhudi za kuudhibiti ugonjwa wa Malaria ambao kulingana na Shirika la Afya duniani unawauwa karibu watu 600,000 kwa mwaka duniani kote wengi wao wakiwa ni watoto.

Katika awamu ya kwanza ya majaribio ya utoaji wa chanjo kwa mwaka 2019 hadi 2023, zaidi ya watoto milioni mbili walipatiwa chanjo ya Malaria aina ya RTS, S kwenye mataifa ya Ghana, Kenya na Malawi. Matokeo yake kulishuhudiwa kupungua kwa wagonjwa wa Malaria na watu wanaolazwa hospitali kutokana na maradhi hayo.

Kulingana na Shirika la Afya duniani WHO, idadi ya vifo imepungua kwa asilimia 13 na sasa linapendekeza chanjo ya RTS s itumike sambamba na chanjo aina ya R21/Matrix-M katika kupambana na Malaria.

Baada ya awamu ya kwanza  kutolewa, chanjo hiyo ilipelekwa kwenye nchi hizo tatu na nyingine 14 ambako ilianzia  Cameroon Januari 2014. Shirika la kimataifa la kuboresha upatikanaji wa chanjo la Gavi limesema tangu wakati huo, dozi nyingine milioni 9.8 zimeshatolewa na kukadiria kuwa takriban watoto milioni tano wamepata kinga kwa kiasi fulani.

Shirika hilo limesema mpango wa utoaji chanjo za Malaria unakusudia kutoa dozi nne za chanjo hizo kwa kila mtoto. Gavi, limepongeza matokeo ya awali ya chanjo hizo nchini Cameroon kwa kufanikiwa kupunguza vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Soma zaidi: Chanjo ya malaria inafanya vizuri Afrika

Mkuu wa Shirika hilo Sania Nishtar ameeleza kuwa katika nchi yenye shida kubwa kama Cameroon ambako ugonjwa huo husababisha vifo vya watoto 13,000 kila mwaka, inawakilisha asilimia 30 ya wagonjwa wote wanaofika hospitali.

Ugonjwa wa Malaria unaambukizwa kupitia mbuPicha: RealityImages/Zoonar/picture alliance

Afrika inaongoza kwa kuwa na asilimia 94 ya wagonjwa wote wa Malaria duniani na asilimia 95 ya vifo vinavyotokana na maradhi hayo kulingana na WHO.

Mwaka 2023, visa milioni 263 vya Malaria viliripotiwa ikilinganishwa na visa milioni 252 kwa mwaka 2022. Hata hivyo, idadi ya vifo vinavyotokana na maradhi yanayoambukizwa na mbu ilipungua kidogo kutoka 600,000 mwaka 2022 hadi 597,000 mwaka 2023. Zaidi ya nusu ya vifo hivyo vilitokea katika nchi nne pekee ambazo ni Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Niger na Tanzania.

Shirika la Gavi limesema linapanga kutanua utoaji wa chanjo kwa nchi nyingine nane zaidi barani Afrika kwa mwaka huu katika juhudi za kuwalinda watoto wengine milioni 13. Limesema kuwa mwaka 2026 hadi 2030 linalenga kuwalinda watoto wengine milioni 50 kwa kugawa dozi nne kwa kila mtoto.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW