GAZA: Chama cha Fatah chaongoza katika matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa
6 Mei 2005Matokeo ya mwanzo yameonyesha Chama cha Fatah cha rais Mahmoud Abbas kimeshinda katika uchaguzi wa serikali za mitaa nchini Palestina. Chama hicho kimeshinda katika miji inayokaliwa na Israel lakini kundi la hamas limefanikiwa kujipatia viti katika miji minne kati ya miji mitano mikubwa.
Kwa mujibu wa Afisa mmoja wa uchaguzi aliyekataa kutajwa jina lake amewambia wanahabari kwamba chama cha Fatah kimeshinda kwa takriban asilimia 60 ya kura zilizohesabiwa.
Habari zaidi zinasema tayari wafuasi wa chama cha Fatah wameanza kusherehekea ushindi katika mji wa Rafah.
Hata hivyo kundi la Hamas limesema ni mapema mno kwao kutabiri kushindwa.
Matokeo ya uchaguzi huo yatatoa changamoto ya mwisho kwa vyama vyote viwili katika uchaguzi ujao wa bunge uliopangiwa kufanyika mwezi July.
Matokeo rasmi ya uchaguzi huo yanatazamiwa kutangazwa jumapili ijayo.