1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMamlaka ya Palestina

Gaza: Matumaini mapya baada ya kufunguliwa Rafah

3 Februari 2026

Matumaini mapya yaangaza Gaza baada ya kufunguliwa kwa kivuko cha Rafah. Huku wagonjwa wakihamishwa kupata matibabu.

Maeneo ya Palestina Khan Yunis 2026 | Majeruhi wa vita na wagonjwa wanasubiri ruhusa ya kutoka kupitia mpakani wa Rafah
Mwanamke aliyembeba mtoto anapanda basi huku Wapalestina—wakiwemo majeruhi wa vita na wagonjwa—wakisindikizwa na ndugu zao, wakijiandaa kuondoka Gaza kupitia mpaka wa Rafah.Picha: Ramadan Abed/REUTERS

Magari ya wagonjwa yanaingia Gaza kuwahamisha Wapalestina wagonjwa na waliojeruhiwa ili kutafuta matibabu nje ya nchi, katika siku ya pili ya kufunguliwa kwa muda kwa kivuko cha Rafah. Kivuko hicho cha mpakani na Misri ndio lango pekee la Gaza kuelekea nje ya ukanda huo mbali na upande wa Israel na ni njia muhimu kwa watu na bidhaa.

Kufunguliwa tena kwa kivuuko hicho ni sehemu muhimu kwenye kile kiitwacho makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na wanamgambo wa Kipalestina, ambayo hata hivyo yamekuwa yakivunjwa mara kadhaa, tangu yalipotangazwa mwezi Oktoba.

Siku ya Jumatatu, kundi dogo la Wapalestina waliojeruhiwa liliweza kuvuka kuelekea Misri. Kwa mujibu wa maafisa wa upande wa Misri idadi ya wagonjwa wanaoruhusiwa kuingia imewekewa ukomo wa watu 50 kwa siku, kila mmoja akiwa na walezi wawili. Hospitali 150 na magari ya wagonjwa 300 tayari yameandaliwa kuwapokea, huku madaktari 12,000 wakitengwa kwa ajili ya kuwahudumia.

Katika Ukanda wa Gaza, mahitaji ya matibabu ni makubwa. Mkurugenzi wa Hospitali ya Al‑Shifa, Mohammed Abu Salmiya, anasema zaidi ya wagonjwa 20,000 wanahitaji matibabu ya haraka, wakiwemo watoto 4,500. Mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel yameripotiwa kusababisha vifo vya makumi ya watu, hali inayoongeza msongamano katika vituo vya afya vilivyodhoofika.

Wito wa Umoja wa Mataifa

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric, amesema kuwa vifaa muhimu vinapaswa kuingia Gaza bila vikwazo:

"Hatimaye, misaada muhimu ya kibinadamu lazima iingie kwa kiwango cha kutosha na kwa masharti machache kupitia Rafah na vivuko vingine vyote. Leo pia, WHO imeunga mkono juhudi za kuwahamisha wagonjwa kutoka Gaza, ingawa kwa kiwango kidogo."

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric asema misaada muhimu ya kibinadamu lazima iingie kwa kiwango cha kutosha Gaza.Picha: Bianca Otero/ZUMA Press/IMAGO

"Kufunguliwa kwa muda kwa kivuko kumeruhusu baadhi ya wagonjwa na walezi wao kutoka moja kwa moja kuelekea Misri, huku wengine wakipitia kivuko cha Kerem Shalom, kinachodhibitiwa na Israel, bila shaka tuna watu wetu upande wa Gaza wanaosaidia Wapalestina wanaorejea. Hata hivyo, kwa kadiri ninavyojua, hatuhusiki na taratibu zozote za uchunguzi au za kiutawala.”

Kwa wakazi wa Gaza ufunguzi wa mpaka wa Rafah umeleta matumaini mapya, si tu kwa wagonjwa, bali pia kwa familia zilizotenganishwa na vita. Wengi wanasubiri kurejea kwa ndugu zao waliolazimika kuondoka Gaza kwa ajili ya matibabu au usalama.

Hata hivyo, hali ya usalama bado ni tete. Gaza imeshuhudia mashambulizi mapya ya anga, huku pande zinazopigana zikiendelea kulaumiana.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW