GAZA: Vyama vya Fatah na Hamas vyatangaza usitishwaji wa mapigano
4 Januari 2007Chama cha Fatah cha rais wa Palestina, Mahmoud Abbas, na chama hasimu cha Hamas, vimetangaza usitishwajiwa mapigano na kukubaliana kubadilishana wafungwa.
Haya yanafuatia kuuwawa kwa watu watano kwenye machafuko yaliyozuka katika Ukanda wa Gaza kati ya vikosi vya vyama hivyo.
Maofisa watatu wa usalama wa chama cha Fatah waliuwawa katika ufyatulianaji wa risasi mjini Khan Younis kusini mwa Ukanda wa Gaza. Mwanamke mmoja mpita njia aliuwawa katika kisa hicho huku watu wengine 12 wakajeruhiwa.
Machafuko hayo huenda yakasababisha hofu ya kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe katika Ukanda wa Gaza.
Wakati huo huo, watu waliokuwa na bunduki walimteka nyara afisa wa serikali ya Palestina mjini Ramallah huko ukingo wa magharibi wa mto Jordan.
Na huko mjini Jenin, watu waliokuwa na bunduki waliishambulia kwa risasi nyumba ya waziri wa magereza wa Palestina, Wasfi Kabha, lakini waziri huyo hakujeruhiwa.