Gaza wasubiri kwa hadhari utekelezaji wa usitishaji mapigano
17 Januari 2025Ikiwa ni Ijumaa ya kwanza tangu kutangazwa kwa makubaliano hayo ya kusitishwa mapigano kulikowatowa Wapalestina mitaani kushangiria matumaini ya hatimaye kupata amani baada ya siku zaidi ya 465 za mauaji na mateso, mitaa iliyokwishabomolewa ya vitongoji vya Khan Younis na kitovu cha Mji wa Gaza inashuhudia pirika za biashara na mikusanyiko ya watu hapa na pale.
Lakini wakati huo huo, ndege za jeshi la Israel zinaendelea na mashambulizi kwenye Ukanda huo, ambapo mamlaka zinasema kuwa hadi jioni ya Alkhamis (Januari 16), siku moja tu baada ya makubaliano kutangazwa, Israel ilishauwa watu 86 kwenye Ukanda wa Gaza.
Soma zaidi: Vifo Gaza vyaongezeka hadi 77 tangu makubaliano yalipofikiwa
Hata hivyo, mashirika ya habari yanaripoti kuwaona watu wakiwa kwenye vifusi vya mitaa na masoko, ingawa wakiwa na tahadhari ya kile kinachoweza kutokea ndani ya masaa 24 yajayo, baada ya baraza la mawaziri la Israel kutoa uamuzi wake wa ama kuyaridhia au kuyakataa makubaliano hayo.
Baraza la mawaziri lakutana
Baraza hilo la mawaziri linaloongozwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu linakutana Ijumaa ya leo, huku kukiwa na shinikizo la jamaa za watu wanaoshikiliwa mateka kulitaka baraza hilo kutokupoteza fursa hii.
Kufuatia migawanyiko ya muda mrefu miongoni mwa wajumbe wa baraza hilo, Netanyahu aliuakhirisha mkutano huo uliokuwa ufanyike Alkhamis, na badala yake kuilaumu Hamas kwa madai ya kurudi nyuma kwenye utekelezaji wa makubaliano, shutuma ambazo Hamas ilizikanusha papo hapo.
Soma zaidi: Netanyahu akabiliwa na shinikizo la kuidhinisha makubaliano
"Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amejulishwa na timu ya upatanishi kwamba makubaliano yamefikiwa juu ya mkataba wa kuwaachia huru mateka." Ilisema taarifa iliyotolewa siku ya Ijumaa (Januari 17) na Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel.
Kabla ya kikao cha baraza zima la mawaziri, kulitarajiwa kifanyike kikao cha baraza la usalama, na hakukuwa na uhakika baraza zima la mawaziri lingekutana Ijumaa ama Jumamosi, ambayo siku moja tu kabla ya muda wa kuanza kwa utekelezaji wa usitishaji mapigano kwa mujibu wa maelezo ya wapatanishi wakuu wa mzozo huu, Qatar na Marekani.
Marekani ina matumaini
Msemaji wa Ikulu ya White House, John Kirby, alisema Washington inaamini kuwa "makubaliano yako kwenye njia sahihi na usitishaji mapigano utaanza kama ulivyopangwa mwishoni mwa wiki hii."
Kundi la wawakilishi wa familia za mateka wa Israel, ambao 33 kati yao wanatakiwa kuachiliwa huru kwenye wiki ya kwanza ya usitishaji mapigano, limemtaka Netanyahu kuharakisha kuyathibitisha makubaliano hayo.
Soma zaidi: Kundi la Hamas limesema linalenga kutekeleza makubaliano ya amani baina yao na Israel
"Kwa mateka 98, kila usiku mmoja ni usiku mwengine wa balaa. Usichelewe kuwarejeshea japo usiku wao mmoja wa ziada." Lilisema tamko lililosambazwa na kundi hilo kwa vyombo vya habari.
Reuters,AFP