1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Gaza:Hakuna njia ya kutoka kwa Wapalestina wenye uraia pacha

30 Oktoba 2023

Wakati mzozo wa Israel na kundi la Hamas ukiingia wiki ya nne, Wapalestina wenye uraia wa nchi mbili wameshindwa kuondoka Gaza kutokana na Israel kuendelea kufunga mipaka na vivuko vya kutokea.

Mpalestina mwenye uraia wa Ujerumani
Mwanamke wa Kipalestina mwenye uraia wa UjerumaniPicha: Abed Rahim Khatib/dpa/picture alliance

Asia Mathkour amekuwa akisubiri kwa shauku taarifa za kufunguliwa kwa kivuko cha mpakani cha Rafah cha kuingia Misri ambacho kingewaruhusu watu kuondoka Gaza. Mwanamke huyo ambaye ni mama wa watoto wawili wadogo,ni Mpalestina mwenye uraia wa  Canada na ameishi na familia yake huko Gaza tangu mwaka 2014. Lakini hadi sasa wameshindwa kuondoka katika uwanja wa vita. Anasimulia kwamba "wiki mbili zilizopita nilipokea simu kutoka kwa Wacanada na kuniambia kwamba kivuko cha Rafah huenda kikafunguliwa na kwamba tunapaswa kwenda hapo". Lakini matumaini yake yalizimika baada ya Israel kuendelea kukifunga kivuko hicho. Soma kuhusu: Maelfu ya watu wapora vituo vya misaada Gaza, yasema UN

Hadi sasa hakuna nchi ambayo imeweza kuwaondoa raia wake au wale wenye uraia wa nchi mbili kutoka Gaza ambayo imekuwa chini ya mashambulizi ya Israel kwa zaidi ya wiki tatu. Maafisa wa Ujerumani wamesema kwamba wapo mamia ya Wapalestina wenye uraia wa Ujerumani mjini Gaza,wengi wakishikilia uraia wa nchi mbili, bila ya kutaja takwimu maalumu. Ikulu ya Marekani ya White House ilisema Rais Joe Biden alifanya mazungumzo tena na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuhakikisha upitaji salama wa raia wa kigeni na Wapalestina wenye uraia wa nchi mbili.

Wapalestina wakisubiri kuvuka na kuingia Misri katika kivuko cha RafahPicha: Fatima Shbair/AP Photo/picture alliance

Lakini kivuko cha Rafah ambacho kwa hivi sasa ndio ujia pekee ya kutoka eneo hilo bado kimefungwa. Kivuko hicho kimefunguliwa tu kuruhusu malori yaliyobeba misaada ya kiutu kuingia Ukanda wa Gaza kutokea Misri. Israel ilifunga vivuko vyake vyote na Gaza baada ya shambulizi la kigaidi lililofanywa na Hamas Oktoba 7 na kuwaua Waisrael zaidi ya 1,400 katika maeneo ya kusini yaliyo karibu na Ukanda wa Gaza. Watu wengine wapatao 229 wanashikiliwa mateka huko Gaza.

Katika kujibu shambulizi la Hamas, Israel imeipiga Gaza kwa mashambulizi ya anga na mizinga kwa wiki kadhaa. Kwa mujibu wa mamlaka ya afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas,mashambulizi ya anga ya Israel yameua zaidi ya watu 7,000. Hamas inatambuliwa kama shirika la kigaidi na Umoja wa Ulaya, Marekani, Ujerumani na nchi nyinginezo.

Mathkour na familia yake walikuwa wakiishi katika eneo la kaskazini mwa mji wa Gaza, karibu na mpaka wa Israel. Vita vilipoanza, familia hiyo ilihamia haraka katika hoteli moja katikati ya Gaza, eneo ambalo lilizingatiwa kuwa salama katika mapigano ya hapo awali. Baadae wanajeshi waliwaeleza Wapalestina waondoke majumbani mwao kaskazini na kuelekea upande wa kusini mwa Ukanda huo.

Wapalestina wakikagua jengo lililoharibiwa na mashambulizi ya IsraelPicha: Said Khatib/AFP

Katika mji wa kale ulionyakuliwa na Israel wa Jerusalem Mashariki, mpishi wa Kipalestina anayeitwa  Izzeldin Bukhari yeye pia ana wasiwasi kuhusu ndugu zake walioko Gaza, akiwemo dada yake. "Sote tuna wasiwasi mkubwa kuhusu kile kinachotokea Gaza. Akili na roho viko Gaza," alisema Bukhari. Ndugu zake wengi wanaishi Gaza, lakini hajawahi kuwatembelea kwa zaidi ya miaka 16. Israel na kwa kiasi fulani Misri zimekuwa zikidhibiti eneo linalotawaliwa na Hamas na hivyo huwa ni vigumu kwa Wapalestina kutoka Jerusalem Mashariki au Ukingo wa Magharibi kupata kibali kutoka mamlaka za Israel cha kuingia Gaza.

Fuatilia habari hii: Israel inasema Wapalestina 700,000 bado wapo kaskazini Gaza

Familia yake ilikuwa ikiishi katika kitongoji cha Rimal katikati mwa mji wa Gaza, ambako kumeshambuliwa vibaya katika vita vinavyoendela. Anasimulia kwamba shangazi yake aliuawa wakati akijaribu kukimbia mara tatu lakini kulikuwa na mashambulizi mengi na hivyo ikawapasa warejee nyumbani. Familia ya Bukhari iliekelea kusini mwa Ukanda wa Gaza lakini mawasiliano na ndugu zake yamekuwa magumu kwasababu ya kukatwa huduma ya kwa umeme na kuharibiwa miundombinu.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW