1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gazeti la The Guardian ladokeza Tsvangirai kuchukua madaraka makubwa Zimbabwe

7 Julai 2008

-

LONDON

Gazeti la The Guardian la Uingereza leo limechapisha taarifa kuhusu Zimbabwe zinazosema kwamba rais Robert Mugabe atabakia kuwa kiongozi wa dola lakini mamlaka kamili yatachukuliwa na kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai kama waziri mkuu kwa mujibu wa mpango uliopendekezwa na rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini.Taarifa hizo zikinukulu duru za uongozi wa juu wa chama cha MDC zimedokeza kwamba rais Mugabe atabakia kuwa rais hadi pale suala la katiba mpya litakapojadiliwa na kuafikiwa na uchaguzi mpya kufanyika.Hata hivyo taarifa hizo hazijatoa maelezo juu ya jibu la rais Mugabe kuhusu pendekezo la Mbeki.Jumamosi rais Mbeki ambaye ni mpatanishi katika mzozo wa kisiasa wa Zimbabwe alikutana na rais Mugabe mjini Harare pamoja na viongozi wa chama cha MDC kilichojitenga kinachoongozwa na Arthur Mutambara.Wakati huohuo Uingereza imetaka hatua kali zichukuliwe pamoja na kukemewa rais Robert Mugabe kutokana na ukaidi wake na kuleta mgawanyiko miongoni mwa wapinzani wake.Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza David Milliband ameitolea mwito Afrika Kusini pamoja na jumuiya nzima ya kimataifa kushikamana katika kuunga mkono azimio kali la Umoja wa mataifa ambalo linataka vikwazo vya kimataifa dhidi ya rais huyo wa Zimbabwe.