Gbagbo aendelea na ubishi wake wa kukataa kung'atuka madarakani nchini Cote d'Ivoire
5 Januari 2011Mazungumzo ya kutafuta suluhisho la mvutano wa kisiasa huko Cote d'Ivoire yataendelea huo ndio msimamo uliofikiwa na wasuluhishi wa mgogoro huo,yaani Umoja wa Afrika na jumuiya ya ECOWAS.Hata hivyo hatua ya kijeshi katika kuung'oa mzizi wa fitna nchini humo haijawekwa pembeni.Pamoja na hilo pia sasa wasuluhishi wanasema rais anayeng'ang'ania madaraka Laurent Gbagbo atapewa msamaha ikiwa atang'atuka kwa hiari uongozini.
Umoja wa Afrika na jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Magharibi mwa Afrika Ecowas zimetoa taarifa inayotilia mkazo wa kuzingatiwa zaidi suluhisho la kidiplomasia katika mgogoro huo wa kisiasa nchini Cote d'Ivoire ikiwa na maana kwamba kutafanyika mazungumzo mengine ya ngazi ya juu hivi karibuni na pande zote mbili zinazovutana nchini humo.Raila Odinga ambaye ni waziri mkuu wa Kenya atawasilisha ripoti yake kuhusu kile kilichojadiliwa na pande zinazovutana kwa mwenyekiti wa tume ya Umoja huo wa Afrika Jean Ping.Aidha ripoti hiyo itatumiwa na Umoja huo katika kuamua ikiwa pana haja ya kufanyika mazungumzo na lini yafanyike. Lakini kabla ya kuondoka Abidjan Raila Odinga amewaambia waandishi wa habari kwamba amempasha bayana bwana Gbagbo kwamba asitegemee kupitishwa suala la kugawana madaraka kama ilivyotokea Kenya,ila anapaswa kufikiria kuanza kuondoka kwa hiari madarakani.Tukinukulu maneno ya waziri mkuu Raila Odinga amesema
''Suluhisho lililochukuliwa katika mgogoro wa Kenya limekuwa ni mtindo unaotegemewa na watu wanaoshindwa katika chaguzi na wanataka kubakia madarakani wakiwa na matumaini ya kutaka kugawana madaraka na upinzani.Suala hilo nimeshamweleza Gbagbo kwamba halitowezekana na wala sio suluhisho katika mgogoro huu.Ikiwa utaratibu huo ndio utakaofuatwa basi utatatiza mpango mzima wa Demokrasia katika bara hili.''
Umoja wa Afrika na jumuiya ya Ecowas zinasema kwamba hatua kidogo imepigwa katika mazungumzo ya kutafuta suluhisho la mgogoro huo wa kisiasa nchini Cote d'Ivoire lakini kwa upande mwingine Gbagbo haonyeshi dalili za kusalimu amri,majeshi yake yanaendelea hadi wakati huu kuizingira hoteli wanayokaa wanasiasa wa kambi ya bwana Quattarra ambayo inalindwa na wanajeshi wa Umoja wa Mataifa.Vizuizi vya kuingia katika Hoteli hiyo viko pale pale,hakuna anayeruhusiwa kuendesha gari kuingia eneo hilo.
Wakuu wa kijeshi wa nchi za jumuiya ya Ecowas wameshaweka tayari mipango ya kumfurusha Gbagbo madarakani ikiwa mazungumzo yatashindwa,na hilo limethibitishwa pia na rais wa wa jumuiya hiyo James Victor Gbeho aliyesisitiza kwa kusema.
''Hatua ya kijeshi bado iko katika mpango wetu na huo ndio msimamo wa Ecowas uliotolewa hapo awali na mpaka sasa tunashikilia msimamo huo''
Fauka ya hayo Alassane Quattarra ambaye anaungwa mkono na jumuiya nzima ya kimataifa akionekana kuridhia hatua hiyo ya ECOWAS amesema kwamba ikiwa hilo litafanyika haina maana kwamba nchi hiyo itatumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Pamoja na kwamba Quattara anataka suluhisho la kidiplomasia katika kuumaza mgogoro huo hataki kukaa meza moja na Laurent Gbagbo. Halikadhalika nchini humo Umoja wa Mataifa umelalamika kwamba rais Gbagbo ameanzisha kampeini chafu za vyombo vya habari dhidi ya chombo hicho. Kituo cha RTI ambacho kinasadikiwa kuwa ni mdomo wa Gbagbo kwa muda sasa kimekuwa kikiwaonyesha watu wawili waliojeruhiwa na kutangaza walipigwa risasi na wanajeshi wa Umoja huo jambo ambalo linakanushwa na jeshi hilo.
Mwandishi Saumu Mwasimba
Mhariri Josephat Charo.