Gebremichael: Bado vikosi vya TPLF vinapambana Tigray
30 Novemba 2020Katika ujumbe wa simu kwa shirika la habari la Reuters Debretsion Gebremichael, anayeliongoza kundi la waasi la TPLF amekanusha ripoti kuwa amekimbilia Sudan Kusini na kusema bado yupo Tigray anakopambana na wavamizi akimaanisha vikosi vya serikali ya Ethiopia. Kiongozi huyo amesema vikosi vyake pia vimewateka wapiganaji wa Eritrea wanaopigana kwa kushirikiana na wanajeshi wa serikali kuu ya Ethiopia. Amesema vikosi vyake bado vipo imara.
"Tumesema mara kwa mara tutapambana kwa kuwashambulia maadui zetu popote walipo na tutapambana na mbinu zetu sio zile maadui zetu wanazotuchagulia, shughuli zetu ni za kukomboa miji iliyotwaliwa, tunapambana na bado tuko imara," alisema Debretsion Gebremichael.
Kwa upande wake Billene Seyoum, msemaji wa Waziri Mkuu Abiy Ahmed amesema matamshi ya Gebremichael, yanapaswa kupuuziliwa mbali.
soma zaidi:Ethiopia: Makombora yarushwa kuelekea nchi jirani ya Eritrea
Hata hivyo hapajakuwa na tamko lolote kutoka kwa serikali ya Eritrea kuhusiana na mapambano yanayoendelea lakini awali ilikanusha vikali kujihusisha na mvutano unaoshuhudiwa kwa sasa. Kundi la waasi la TPLF hivi karibuni lilivurumisha makombora katika mji mkuu wa Eritrea Asmara.
Madai ya pande zote zinazohasimiana ni vigumu kuthibitisha kutokana na kwamba huduma za simu na mitandao zimetatizwa huku simu zikifuatiliwa tangu vita vilipoanza Novemba 4.
Abiy Ahmed asema kamwe hawatausambaratisha mji wa Mekelle
Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ameliambia bunge leo Jumatatu kwamba wanajeshi wa serikali hawajasababisha kifo cha raia yeyote takriban mwezi mmoja tangu walipoanza mapambano yao dhidi ya kundi la TPLF katika jimbo la Tigray.
Abiy pia amesema jeshi lake halitausambaratisha mji mkuu wa Tigray Mekelle baada ya kuudhibiti hapo jana.
Vita katika jimbo la Tigray hadi sasa vimesababisha vifo vya maelfu ya watu, mamilioni kukosa makaazi na takriban wakimbizi 44,000 wakikimbilia nchini Sudan Eritrea na Somalia na kusababisha pia mvutano kati ya makundi ya kikabila nchini Ethiopia.
Zaidi soma hapa: Jeshi la Ethiopia katika 'hatua ya mwisho' ya mashambulizi Tigray
Huku hayo yakiarifiwa mkuu wa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa Filippo Grandi amesema hata baada ya serikali kuu ya Ethiopia kutangaza kumaliza operesheni yake ya kijeshi katika jimbo la Tigray hii haimaanishi kuwa mgogoro huo umemalizika.
Amesema ana wasiwasi juu ya hatima ya wakimbizi wa Eritrea hasa habari kuwa baadhi yao wametekwa.
Takriban mwezi mmoja wa mapigano kati ya wanajeshi wa Ethiopia na wale wa jimbo la Tigray yametishia kuiyumbisha Ethiopia na eneo zima la pembe ya Afrika.
Chanzo: Reuters