GENEVA: Iran yaendelea kurutubisha uranium
15 Juni 2007Matangazo
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Kinuklia la Umoja wa Mataifa,IAEA ameihimiza Iran kusitisha mradi wake wa kurutubisha madini ya uranium.Mkurugenzi wa IAEA,Mohamed El Baradei amesema,kutopatikana kwa maafikiano kati ya Iran na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kunazidisha mvutano.Wakati huo huo akasema,kuchukuwa hatua ya kijeshi dhidi ya Iran kutakuwa ni „kitendo cha wazimu.“El Baradei akizungumza mwishoni mwa mkutano wa IAEA ulioshindwa kupata maendeleo yo yote kuhusu mgogoro wa Iran,alisema Iran inaendelea kustawisha teknolojia ya kurutubisha uranium. Serikali za magharibi zina hofu kuwa Iran inajaribu kutengeneza silaha za nyuklia,lakini Tehran inadai kuwa mradi wake wa nuklia ni kwa ajili ya matumizi ya nishati ya nchi hiyo.