GENEVA : Maisha ya watu 54,000 hatarini nchini Congo
5 Machi 2005Machafuko ya umwagaji damu wa kikabila kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo yameweka maisha ya raia 54,000 katika hatari ya kufa au kupata magonjwa.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumiwa Watoto UNICEF watoto,wagonjwa na wazee ndio wanaoweza kuathirika zaidi baada ya mashirika ya misaada kusitisha opresheni zake katika jimbo lisilokuwa na utawala wa sheria la Ituri ambapo watu waliopotezewa makaazi yao wanaishi kwenye makambi baada ya kuyakimbia mapigano katika miezi ya hivi karibuni.
Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wameuwawa watu 50 wakati wa mapambano ya silaha karibu na mji wa Bunia na wapiganaji wanamgambo hapo Jumanne siku tano baada wanajeshi 9 wa Umoja wa Mataifa kutoka Bangladesh kuuwawa katika eneo hilo hilo.Machafuko hayo ya umwagaji damu yamepelekea kujitowa kwa mashirika ya kibinaadamu katika eneo hilo.
Mapigano hususan kati ya makundi ya kikabila ya Walendu na mahasimu wao Wahema yameuwa watu 50,000 katika jimbo la Ituri tokea mwaka 1999.