Geneva: Ujerumani yaahidi kuipa Pakistan Euro milioni 84
9 Januari 2023Nchi hizo ni pamoja na Ujerumani ambayo imeahidi kutoa kiasi cha Euro milioni 84 ambazo ni sawa na dola milioni 90. Umoja wa Ulaya utatoa mchango wa jumla ya dola milioni 87. Naye rais wa Benki ya Kiislamu ya Maendeleo mesema kundi la nchi hizo za Kiislamu litatoa mchango wa dola bilioni 4.2 za kuiwezesha Pakistan kujijenga upya.
Afisa mwandamizi wa Shirika la maendeleo USAID, amefahamisha kuwa Marekani itatoa dola milioni 100 za ziada kwa ajili ya kuipa ahueni Pakistan kutokana na mafuriko makubwa mwaka jana. Akizungumza kwa njia ya video, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliuambia mkutano huo kuwa nchi yake itachangia euro milioni 360 sawa na dola za kimarekani milioni 384.
Mkutano huo wa Umoja wa Mataifa umehudhuriwa ana kwa ana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Waziri Mkuu wa Pakistan Shahbaz Sharif wakati viongozi wengine wa dunia kama vile Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na mwenzake wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan wakishiriki kwa njia ya video huku nchi zote zilizohudhuria mkutano huo zikiweka msisitizo wa kuisaidia Pakistan kukusanya kiasi kinachokadiriwa cha dola bilioni 16.3 zinazohitajika kuisaidia nchi hiyo kujijenga upya.
Kwenye mkutano huo Waziri mkuu wa Pakistan Shahbaz Sharif alisema ni wazi kwamba uwezo wa Pakistan wa kujikomboa kutokana na maafa makubwa ya mafuriko utategemea sana kasi ya mpango na hatua zilizopendekezwa na Umoja wa Mataifa kuweza kurejesha miundombinu muhimu na kufufua ukuaji wa uchumi haraka. Sharif amesema jambo la muhimu zaidi ni muitikio wa kuifadhili Pakistan kifedha. ameongeza jkusema kwamba ikiwa pengo la kupatikana fedha litaendelea kutatiza juhudi za serikali yake na kushindwa kuyatimiza mahitaji kwa uthabiti, basi matokeo yanaweza kuwa mabaya sana.
Shehbaz Sharif, amesema Pakistan inahitaji dola bilioni 8 kutoka jumuiya ya kimataifa katika kipindi cha miaka mitatu ijayo kuunga mkono juhudi za kujijenga upya baada ya mafuriko yaliyosababisha vifo vya takriban watu 1,700 na mamilioni ya watu walipoteza makazi yao Pamoja na uharibifu mkubwa wa miundombinu.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa kufanyika mageuzi makubwa kwenye mfumo wa fedha wa kimataifa ili kuziwezesha nchi zenye kipato cha chini kupata ufadhili wa kutosha kutoka kwa mataifa tajiri pale nchi hizo zitakapokabiliwa na majanga ya hali ya hewa. Guterres ameulaumu mfumo wa sasa wa fedha duniani amesema ni wa upendeleo kutokana na jkwamba mfumo huo ulibuniwa na kundi la nchi tajiri na hivyo ni nchi hizo tu ndio zinazonufaika.
Vyanzo:AP/DPA/RTRE/