GENEVA:Iran yakubali kuendelea kusimamisha mpango wa Nuklear na kukubaliwa tena kwa mazungumzo na WTO
26 Mei 2005Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wamesema wamepusha matatizo na Iran juu ya mpango wake wa Nuklear.
Katika mkutano wa Geneva mawaziri wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani wamekubaliana na Iran kwamba itaendelea kusimamisha kwa muda mpango wake wa kurutubisha madini Uranium huku kukisubiriwa kufanyika mazungumzo mengine katika kipindi cha msimu huu wa joto.
Makubaliano hayo yamesababisha suala hilo la Iran kutofikishwa mbele ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ili kujadili uwezekano wa kuwekewa Vikwazo..
Wakati huo huo Shirika la biashara duniani WTO limekubali kuanza mazungumzo ya kuipa uanachama Iran baada ya Marekani kubadili msimamo wake wa muda mrefu kupinga Iran kuwa mwanachama wa WTO.
Serikali ya Marekani inaishutumu Iran kwa kutengeneza silaha za Nuklear wakati Iran inasisitiza kwamba mpango wake wa Nuklear ni kwa ajili ya matumizi yake ya amani.