1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

George Forrest: Uhusiano wangu na Katumbi si wa kisiasa

23 Februari 2018

Mfanyabiashara wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo George Malta Forrest amezungumzia juu ya utajiri wake na kusisitiza wake uhusiano wake na mpinzani wa Rais Joseph Kabila, Moise Katumbi si wa kisiasa.

Kongo Oppositionspolitiker Moise Katumbi
Moise Katumbi, rafiki wa muda mrefu wa ForrestPicha: Getty Images/AFP/F. Scoppa

Mfanyabiashara wa Jamhuri ya kidemokrasia ya kongo George Malta Forrest amezungumzia  juu ya utajiri wake na kusisitiza kuwa uhusiano wake na mpinzani wa Rais Joseph Kabila Moise Katumbi si wakisiasa. Forrest aliwahi kuwa Mkuu wa kampuni ya uchimbaji madini ya serikali chini ya utawala wa Rais wa zamani wa nchi hiyo Laurent Kabila.

Muda mfupi kabla ya Rais wa zamani wa Congo Laurent kabila kufanya mashambulizi ya mwisho ya ushindi dhidi ya kinshasa, alipita Lubumbashi na kukutana na mjasiriamali ambaye jina lake halikuwa geni masikioni mwake. Baada ya kusalimiana inasemekana waliweka miadi ya kukutana baadaye.

Mara baada ya kuingia madarakani Kabila hakumwangamiza Forrest kama ambavyo Mobutu alimfanyia baba yake kwa kuzuia magari yake kufanya kazi. Badala yake, Kabila alimteua kuwa mkuu wa Kampuni ya uchimbaji madini ya serikali ya Gecamines, inayotumika kuchimba madini ya nchi yake na kutajirisha maafisa wa serikali.

Forrest anasema, alifikia makubaliano na kabila kuwa kila mwezi Kampuni ya Gecamines ingehamisha dola za kimarekani milioni nne kwenda benki kuu.

Madini ya kobalti yanayochimbwa kwa wingi DRCPicha: Amnesty International/Afrewatch

Baada ya kuuawa kwa Kabila mwaka 2001 mwanaye, Rais wa sasa Joseph Kabila aliingia madarakani na mfanyabiashara Forrest alijiuzulu cheo chake kwenye kampuni ya Gecamines na kurejelea biashara zake. Kadri muda ulivyozidi kusonga, ndivyo mashirika yasiyo ya kiserikali yalivyozidi kumtuhumu Forrest kupora madini na kufanya biashara haramu ya silaha, tuhuma ambazo alizikanusha.

Forrest amesema siku zote amekuwa mtu safi na kwamba mashirika yasiyo ya kiserikali yana mshambulia kwasababu hajayapa ufadhili. Mnamo mwaka 2017,serikali ya China ilikubali kuipa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo mabilioni ya dola, kwa ajili ya kuboresha miundo mbinu na uchimbaji madini.

Hii ilimaanisha kwamba, ni lazima Forrest arejeshe ardhi yenye madini ya shaba na na kobalti aliyokuwa akimiliki. Forrest amesema wawekezaji wa kichina hutoa mapendekezo ya kuvutia kwa ajili ya Congo bila kujali gharama za malighafi na kwamba jambo hilo si sawa.

Mfanya biashara huyo anayekadiriwa kuwa na utajiri wa dola milioni mia nane na jarida la Forbes kumtaja kushika nafasi ya pili kwa utajiri kwenye nchi za kusini mwa jangwa la sahara amejikita kwenye kuangalia miradi yake mingine ikiwemo benki ya BCDC aliyoinunua kutoka benki ya kifaransa BNP, na zaidi ya ng´ombe 38000 walio kwenye ranchi yake.

Hivi sasa, Forrest mwenye miaka 78 amekabidhi biashara zake kwa mwanaye aitwaye Malta akiongoza kampuni hiyo inayojihusisha na shughuli mbalimbali ikiwemo ujenzi, biashara na nishati mbadala zenye maslahi kwenye nchi za Kenya, Afrika kusini na Ubelgiji.

Kuwepo kwa mgogoro wa kisiasa na shinikizo la kumuondoa Rais aliyeko madarakani, mmoja wa wapinzani wa Rais Kabila ambaye ni gavana wa zamani wa Katanga na mmiliki wa timu ya mpira ya TP Mazembe, Moise Katumbi ni rafiki wa muda mrefu wa Forrest anayeishi uhamishoni mjini Brussels. Forrest anasema urafiki wake na Katumbi sio wa kisiasa.

Mwandishi: Angela Mdungu

Mhariri: Yusuf Saumu