1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

George Weah ashinda uchaguzi wa rais Liberia

Oumilkheir Hamidou
29 Desemba 2017

Furaha na shangwe zimehanikiza mjini Monrovia na nchini Liberia kwa jumla tangu mchezaji nyota wa zamani wa soka ulimwenguni, George Weah kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Liberia Präsidentschaftswahlen Anhänger George Weah
Picha: Reuters/T. Gouegnon

Mara baada ya habari kuhusu ushindi wa George Weah kutangazwa, maelfu kwa maelfu ambao tayari walikuwa wamejazana pembezoni mwa makao makuu ya tume ya uchaguzi waliteremka majiani na kuanza kushangiria."Weah Weah ,tutaandika historia" ni miongoni mwa matamshi yaliyohanikiza usiku kucha. Shabiki mwengine wa George Weah anaongeza: "Hii ni nchi yetu, na sote tunabidi kuungana na kuangalia jinsi tutakavyoweza kuinyanyua nchi yetu.Tuna watoto, tuna baba zetu, jama zetu na ndugu zetu na katika wakati ambapo historia ya miaka iliyopita  kati ya 1991 hadi 2005 ilikuwa mbaya kwetu....sasa tuko katika hali ya furaha na tunasherehekea. Hakuna vita. Namshukuru Mungu kwa kutupatia amani."

Baada ya kuhesabiwa zaidi ya asili mia 98 ya kura jana usiku, George Weah  amejikingia asili mia 61.5 ya kura huku mshindani wake, makamo wa rais Joseph Boakai akijipatia asili mia 38.5 ya kura.

Rais aliyestaafu bibi Ellen Johnson SirleafPicha: T. Charlier/AFP/Getty Images

Zoezi la kwanza la kukabidhi madaraka kwa njia ya kidemokrasia

Liberia, nchi iliyoundwa na watumwa walioachiwa huru nchini Marekani inaingia katika utaratibu wa kwanza wa kubadilishana madaraka kwa njia za kidemokrasia katika kipindi cha zaidi ya miaka 70, baada ya rais wa kwanza wa kike, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, Ellen Johnson Sirleaf, kustaafu.

George Weah mwenye umri wa miaka 51, senetor aliyeingia katika uwanja wa kisiasa baada ya kustaafu katika viwanja vya dimba mwaka 2002, aliongoza, duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais ilipoitishwa Oktoba mwaka huu, lakini hakujikingia wingi wa kutosha wa kura dhidi ya mpinzani wake Boakai mwenye umri wa miaka 73 ambae ametumikia wadhifa wa makamo wa rais kwa kipindi cha miaka 12. Sirleaf hakumuunga mkono mgombea yeyote yule kati ya hao wawili.

Msemaji wa chama cha Boakai, Unity Party, Mohammed Ali amekiambia kituo cha matangazo cha Capital FM kwamba chama chao hakitotuma malalamiko mahakamani kwasababu  wananchi walio wengi wa Liberia wameshaamua.

Wananchi washerehekea ushindi wa mgombea wao George WeahPicha: Reuters/T.Gouegnon

Madaraka yarejea mikononi mwa wananchi

Rais mpya Georg Weah anatazamiwa kukabidhiwa hatamu za uongozi mwezi unaokuja wa Januari. Hakuna, si Weah na wala si Boakai aliyetoa taarifa yoyote hadharani tangu matokeo ya uchaguzi yalipotangazwa jana usiku.

"Tumesubiri miaka 12, sasa madaraka yanawarejea wananchi" amesema makamo mwenyekiti wa ligi ya vijana-mmojawapo wa washirika katika muungano kwaajili ya mageuzi ya kidemokrasi unaoongozwa na George weah na makamo wake, seneta Jewel Howard-Taylor, mke wa zamani wa kiongozi wa zamani wa waasi na rais wa zamani anaeshikiliwa jela, Charles Taylor.

Wachunguzi wa uchaguzi huo wamesema zoezi la uchaguzi lilikuwa la haki na limepita kwa amani.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW