1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoGeorgia

Georgia yaandika historia katika mashindano ya Euro 2024

27 Juni 2024

Georgia iliiduwaza Ureno na kutinga hatua ya mtoano ya mashindano ya ubingwa wa Ulaya - UEFA Euro 2024. Ni ushindi wa kihistoria kwa nchi hiyo ambayo inashiriki kwa mara ya kwanza kabisa katika mashindano makubwa.

Euro 2024 – Georgia – Portugal
Georgia wametinga hatua ya mchujo kwa mara yao ya kwanza katika mashindano makubwaPicha: David Rawcliffe/Propaganda Photo/IMAGO

Waliwafunga mabingwa hao wa zamani wa Ulaya mabao 2 – 0. Ushindi huo wa kushangaza wa Georgia unawapa zawadi ya kukutana na Uhispania Jumapili usiku na una maana walifuzu kama moja ya timu nne bora zilizomaliza katika nafasi ya tatu kwenye makundi, Pamoja na Slovenia, Uholanzi na Slovakia. Uturuki pia ilijiunga nao baada ya kuwatimua Waczech kwa kuwafunga 2 – 1. Sasa watacheza dhidi ya Austria katika hatua ya mchujo Jumanne wiki ijayo.

Soma pia: Ujerumani yafuzu kwa duru ya mtoano kombe la EURO

Awali, Romania, Ubelgiji, na Slovakia zilitinga katika 16 za mwisho huku Ukraine ikipoteza tiketi kwa sababu ya tofauti ya magoli na kuwa timu ya kwanza kutolewa nje ikiwa na pointi nne tangu mashindano hayo kuanza kuchezwa katika muundo wake wa sasa. Katika hali ambayo haijawahi kushuhudiwa, timu zote nne za Kundi E zilimaliza na pointi nne kila mmoja baada ya Ubelgiji na Ukraine kutoka sare ya 0 – 0 mjini Stuttgart na Romania na Slovakia kutoka sare ya 1 – 1 mjini Frankfurt. Ubelgiji itakwaruzana na Ufaransa Jumatatu wakati wapinzani wa Slovakia watakuwa ni England Jumapili.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW