1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mateka wa kijerumani waachiliwa huru.

Liongo, Aboubakary Jumaa21 Julai 2008

Wapanda milima watatu wa kijerumani waliyotekwa na wapiganaji wa PKK nchini Uturuki na ambao waliachiwa hapo jana wanatarajiwa kuwasili hapa Ujerumani leo hii.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ambaye alitangaza kuwa alipumua baada ya kupata habari za kuachiwa kwa mateka wa kijerumani na kundi la PKKPicha: DW

Wapanda milima hao walitekwa mnamo siku 12 zilizopita wakiwa miongoni mwa wapanda milima 13 waliyokuwa wakipanda mlima Atarat  uliyoko katika Jimbo la Agri nchini Uturuki.


Mapema wateka nyara hao wa PKK waliitaka serikali ya Ujerumani kuacha harakati dhidi ya kundi hilo ambalo limewekwa katika orodha ya makundi kigaidi na Umoja wa Ulaya pamoja na Marekani


Wapanda milima hao walikuwa wakitegemewa kuwasili Ankara mchana huu kabla ya kuanza safari ya kurejea nyumbani Munich.


Gavana wa jimbo la Agri Mehmet Cetin aliwaambia waandishi wa habari ya kwamba waasi hao walilazimishwa kuwaachia huru mateka hao baada ya majeshi ya nchi hiyo kuwazingira.


Waliachiwa jana kabla ya kuchukuliwa na polisi katika milima hiyo ya Ararat wakiwa katika hali nzuri.


Waziri Mkuu wa jimbo la Bavaria hapa Ujerumanui Guenther Beckstein alisema kuwa anafurahi kuwa sakata hilo la kutekwa nyara kwa wajerumani hao limemalizika kwa usalama bila ya umwagaji damu.


Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Frank- Walter Steinmeier kwa upande wake aliishukuru Idaraya Usalama ya Uturuki kwa kuchangia hatua hiyo.


Wapanda milima hao Lars Holger Renne,Martin George na Helmurt Johann, waliachiwa huru hapo jana baada ya kuwa katika mikono ya wapiganaji wa PKK kwa siku 12.


Wapiganaji hao walidai kuwa hatua yao hiyo ni kuitaka serikali ya Ujerumani kuacha kile walichosema sera za chuki dhidi yao.


Kundi hilo pia lilitishia ya kwamba litafanya hujuma dhidi ya rasilimali za kiuchumi za Ujerumani zilizoko nchini Uturuki.


Mwezi uliyopita Wizara ya Mambo ya Ndani ya  Ujerumani ilikipiga marufuku kituo cha televisheni cha Kituruki kiitwacho  Roj.TV kwa kile ilichodai kuwa na maingiliano na kundi hilo la PKK.


Kundi hilo la PKK liko katika orodha ya makundi ya kigaidi katika nchi za Ulaya  pamoja na Marekani.


Mwenyekiti wa jumuiya ya waturuki nchini Ujerumani Kenan Kolat alipongeza hatua hiyo ya kuachiwa kwa mateka hao na kusema kuwa toka mwanzo wa sakata hilo uhusiano kati ya Ujerumani na Uturuki ulizidi kuimarika.