Ghana na namibia-kombe la Afrika
23 Januari 2008Wenyeji Ghana wanarudi tena leo uwanjani kwa mpambano wapili wa Kundi A, baada ya jumapili kufungua dimba kwa ushindi wa mabao 2:1 na Guinea.Mahasimu wao ni Namibia iliozabwa mabao 5:1 na Morocco.
Katika mpambano wapili,Guinea ina miadi na Morocco ikiwa na kibarua kwanza kzuwia wembe ulioinyoa Namibia hauinyoi na wao na pili lazima ishinde leo ikiwa haitaki kuaga mashindano tayari duru ya kwanza.
Mohammed Abdulrahman anawafunulia kawa la Kombe la Africa Cup jioni ya leo:
Ghana yaweza leo ikafanya mabadiliko 2 katika kikosi chake- „Black Stars“ kinachopambana na Namibia mjini Accra.
Kocha wao mfaransa Claude Le Roy ametaja kwamba beki wao wa kati ya uwanja John Mensah na mwenzake John Paintsil, pengine wasiweze kucheza.Isitoshe, Shilla Illiasu anaecheza dimba huko Russia, hakupona bado maumivu yake ya goti yaliosababisha asicheze jumapili pale Ghana ilipoikomea Guinea 2-1.
Hatahivyo, Black Stars hawakusudii leo kuregeza kamba .Kwani, wakishinda tena leo, basi watatia mfukoni tiketi yao ya duru ijayo ya robo-finali.
Kocha wa Ghana Le Roy, anamtazamia tena Sulley Muntari kuiokoa tena Ghana kama alivyofanya jumapili iliopita kwa bao lake la dakika ya mwisho.
Na ushindi wapili leo unaweza tena ukazusha mtafaruku na shamra shamra katika mitaa ya jiji kuu Accra kama jumapili iliopita .Kuepusha balaa jengine,serikali nchini Ghana jana iliwataka mashabiki wa Black Stars kumtuliza shetani na hasa baada ya shabiki mmoja kuuwawa usiku wa jumapili iliopita kufuatia ushindi dhidi ya guinea.
Maalfu ya mashabiki walitamba majiani mjini Accra ,wakichoma moto mipira ya magari huku wengine wakiendesha motokaa kwa kasi ,wakipiga honi na kupepea bendera za nyota nyeusi.
Vyombo vya habari nchini Ghana, viliripoti jana kwamba shabiki mmoja wa miaka 25 alijeruhiwa vibaya pale pikipiki akiendesha ilipogonga gari lilioegeshwa.Alifariki baadae hospitali.
Namibia,inahitaji ushindi leo kufuta madhambi ya mpambano wao wa kwanza walipokandikwa mabao 5-1 na simba wa Atlas-Morocco.
Morocco na Guinea zinakumbana pia leo Katika kile ambacho wengi wanakiona ni „marudio ya finali ya kombe la Afrika la mataifa 1976“ mjini Addis Ababa, Morocco iliilaza Guinea dakika ya mwisho na leo kwa guinea ni kulipiza kisasi.Maandalio ya simba wa Atlas kwa changamoto hii yalipatwa na mkosi kwa kuumia kwa mshambulizi wao hatari Soufiane Alloudi. Kwani yeye alikuwa „alloudi“ ya kweli siku Morocco ilipofungua dimba na Namibia.Alitia jumla ya mabao 3 pekee.
Kwa jinsi walivyotamba majuzi, wamorocco waonesha wameuzika msiba uliowapata katika kombe lililopita 2006 nchini Misri walipotolewa duru ya kwanza tu.Sasa wanazungumzia kurejea ushindi wa ile timu yao ya 2004 huko Tunisia ilipoibuka makamo-bingwa.
Kwa Guinea na Namibia, zilizoshindwa mpambano wao wa kwanza,leo ni „kufa-kupona“.Pigo jengine ,itakua kufunga virago na mapema kurudi Conackry na Windhoek.