1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghana yafungasha virago michuano ya AFCON

19 Januari 2022

Michuano ya soka barani Afrika AFCON iliendelea kutimua vumbi usiku wa kuamkia Jumatano kwa michezo kadhaa ikiwemo kati ya timu ya taifa ya Ghana na visiwa vya Commoro uliomalizika kwa Ghana kukubali kichapo cha bao 3-2.

Africa Cup of Nations Ghana vs Komoren
Picha: Daniel Beloumou Olomo/Getty Images/AFP

Ghana, washindi mara nne wa michuano ya AFCON walikabana koo na timu ya taifa ya visiwa vya Commoro inayoshiriki kwa mara ya kwanza fainali za kandanda barani Afrika. Mashabiki wa Ghana hawakuamini macho yao baada ya kukubali kichapo hicho cha bao 3-2 kutoka kwa Commoro.

Huo ulikuwa ni mwelendelezo wa maajabu yanayoshuhudiwa kwenye michuano hiyo ya AFCON inayoendelea nchini Cameroon.

Siku mbili baada ya Algeria inayotetea kombe kwenye michuano hiyo kuambulia kipigo kutoka kwa Guinea ya Ikweta, anguko la Ghana katika mchezo wa Jumanne jioni ulitoa taswira ya kuibuka kwa vigogo wapya wa mchezo wa soka barani Afrika.

Katika mchezo huo uliojaa misukosuko, Ghana iliachwa nyuma katika dakika nne za kwanza za mchezo kwa kuruhusu bao la kwanza la Comoro. Mambo yaliwachachia zaidi mnamo dakika ya 25 baada ya nahodha wake Andre Ayew kulambishwa kadi nyekundu. Hadi dakika 61 ya mchezo Commoro walikuwa wakiongoza kwa bao 2-0.

Ghana yaondoka Cameroon kichwa chini 

Mwamuzi Boubou Traore akimwonesha kadi nyekundu mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ghana Andre Ayew Picha: Daniel Beloumou Olomo/Getty Images/AFP

Ghana ilifanikiwa kusawazisha kwa kupachika wavuni mabao 2 dakika 13 kabla ya kukamalizika kwa mtanange huo. Hata hivyo hata kabla ya kushusha pumzi vizuri mshambuliaji wa Comorro Ahmed Mogni aliwalambisha kaa la moto mnamo dakika ya 85 kwa kupachika wavuni bao lake la pili kwenye mchezo huo na kuiwezesha timu yake kuibuka kidedea filimbi ya mwisho ilipopulizwa.

Matokeo hayo yameilazimisha Ghana kuyaaga mashindano ya AFCON wakiwa washika mkia katika kundi msimamo wa kundi C. Kwa muda mrefu Ghana imekuwa kiniara wa mchezo wa soka barani Afrika na imefanikiwa kutinga walau hatua ya nusu fainali katika michuano 6 kati ya saba iliyotangulia.

Ni mara ya mwisho kutolewa katika hatua ya makundi ilikuwa mnamo mwaka 2006. Licha ya kuwa na wachezaji vigogo kutoka klabu kubwa duniani Ghana haikufurukuta mbele ya Commoro ambaye mchezaji wake macharari Ahmed Mogni anachezea ligi daraja la tatu nchini Ufaransa.

Morocco na Gabon yasonga mbele hatua ya mtoano 

Katika mchezo mwingine uliopigwa jana, Morocco ilifanikiwa kuwa kileleni mwa kundi C kufuatia mchezo kati yake na Gabon uliomalizika kwa sare ya bao 2-2.

Morocco ambaye ilikwishafuzu kwenda hatua ya mtoano ilijinyakulia pointi moja ya nyongeza goli la kusazisha la dakika za lala salama lililofungwa na mshambuliaji wake anayekipiga kwenye klabu ya Paris Saint-Germain ya nchini Ufaransa Achraf Hakimi.

Wachezaji wa timu ya taifa ya MoroccoPicha: AFP via Getty Images

Kwenye mchezo huo Gabon iliwakosa nyote wake watatu ikiwemo nahodha wao Pierre-Emerick Aubameyang  na kiungo wa kati Mario Lemina waliorejeshwa kwenye klabu zao kwa vipimo zaidi baada ya kupata athari kutokana na kuambukiza virusi vya corona. Kiungo wake mshambuliaji Denis Bouanga hakuweza kucheza hiyo jana baada ya naye pia kuambukizwa Covid-19.

 Matokeo hayo yanaiwezesha Gabon kusonga mbele katika hatua ya 16 bora.. Commoro kwa upande wake watasubiri maajaliwa ya kuingia hatua ya mtoano kupitia dirisha la timu bora za nafasi ya tatu. Itatakiwa hata hivyo kusbiri kuona timu kutoka makundi mengine zinafanya vipi katika michezo ya kukamilisha hatua ya makundi.

Hapo mapema timu ya taifa ya Senegal ilifuzu hatua ya mtoano baada ya kuongoza kwa alama za kundi B licha ya sare ya bila kufungana katika mchezo wake dhidi ya Malawi.

Zimbabwe ambayo tayari ishayaaga mashindano hayo iliwashangaza wengi kwa kuichabanga Guinea bao 2-1 kwenye mchezo mwingine wa kundi B.

Hadi sasa timu saba zimekwishatangulia kwenye hatua ya mtoano. Timu nyingine zitaamuliwa kwenye michezo ya mwisho ya makundi itakayopigwa leo Jumatano na kesho Alhamisi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW