1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghana yataka kuhakikishiwa usalama Misri

5 Novemba 2013

Ghana imeliomba Shirikisho la Soka Ulimwenguni liandae mkutano wa dharura kuhusiana na mipango ya usalama ya mchuano wa mchujo wa kufuzu katika fainali za kombe la dunia dhidi ya Misri mjini Cairo.

Kikosi cha Kandanda cha Timu ya Taifa ya Ghana
Kikosi cha Kandanda cha Timu ya Taifa ya GhanaPicha: imago

Waziri wa Michezo wa Ghana Elvis Afriyie Ankrah amemwandikia barua Katibu Mkuu wa FIFA Jerome Valcke akisisitiza kuhusu wasiswasi wa nchi yake kuhusiana na usalama wa wachezaji na maafisa watakaosafiri kwenda Cairo kwa mchuano huo wa Novemba 19 ambao FIFA iliamuru uandaliwe mjini humo.

Takribani mashabiki 30,000 huenda wakahudhuria mechi hiyo, ambayo ni ya kwanza kabisa ya kimataifa kuchezwa mjini Cairo katika miaka miwili na mchuano wa kwanza wa nyumbani unaoihusisha Misri, ambako aina hiyo ya kiasi kikubwa cha watu kitakubaliwa uwanjani tangu machafuko yaliyozuka wakati wa mpambano mjini Port Said mwaka 2012 ambapo watu 70 waliuawa. Huo ndio uliokuwa mkasa mbaya zaidi kuwahi kutokea katika mchezo wa kandanda ulimwenguni.

Wizara ya michezo ya Ghana inasema ilikubali uamuzi wa FIFA ijapokuwa haikufurahia sana, lakini imeomba maelezo zaidi kuhusu hakikisho la usalama lililotolewa na maafisa wa Misri na kuifanya FIFA kuamua mechi hiyo ichezwe mjini Cairo. Pia inataka kujua nani atakayewajibika kama kutatokea tukio lolote la utovu wa nidhamu au matatizo mengine.

Ili kuwasaidia wachezaji kutokabiliwa na mazingira ya kutoa hofu, kikosi cha Ghana kitakita kambi nchini Ethiopia kwa wiki moja na kuwasili mjini Cairo siku moja tu kabla ya kushuka dimbani. FIFA iliamuru wiki iliyopita kuwa mechi hiyo inaweza kuendelea baada ya kuridhishwa na hakikisho lililotolewa na maafisa wa Misri, ambao wataandaa mpambano huo katika uwanja unaomilikiwa na jeshi wa Juni 30.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW