Ghasia nchini Misri Udugu wa Kiislamu waitisha maandamano zaidi
17 Agosti 2013Waandamanaji wa Udugu wa Kiislamu wanapinga kuondolewa madarakani kwa Mohammed Mursi na ukandamizaji uliosababisha umwagikaji mkubwa wa damu.
Mapigano makali kabisa ya mitaani ambayo hayajawahi kuonekana mjini Cairo katika muda wa zaidi ya miaka miwili ya ghasia yamesababisha kiasi watu 82 kuuawa, ikiwa ni pamoja na maafisa wa polisi.
Mapambano ya silaha
Wakaazi wamekuwa wakifyatuliana risasi na kuashiria mwelekeo mbaya katika mzozo huo, wakati raia ambao walikuwa na bastola na bunduki walipopambana na waandamanaji waliokuwa wakishiriki kile ambacho kundi la Udugu wa Kiislamu ilikiita "siku ya hasira" , iliyozushwa na hasira dhidi ya majeshi ya usalama kuwaondoa kwa nguvu waandamanaji waliokuwa wamekita kambi katika maeneo mawili mjini Cairo siku ya Jumatano na kuzusha mapambano ya nchi nzima ambapo watu zaidi ya 600 walipoteza maisha.
Helikopta za jeshi zilizunguka hewani wakati wakaazi wakiwa na hasira dhidi ya maandamano ya Udugu wa Kiislamu wakiwatupia mawe na chupa waandamanaji. Pande hizo mbili pia zilifyatuliana risasi, na kuzusha mapambano katika mitaa katika maeneo yanayokaliwa na watu katika vitongoji vya mji huo.
Maandamano zaidi
Udugu wa Kiislamu wakionyesha ukaidi wameitisha wiki ya maandamano nchini Misri kuanzia leo Jumamosi.Majeshi ya usalama na raia kadhaa waliuzingira msikiti wa al-Fateh katikati ya jiji la Cairo katika eneo la Ramses ambako waandamanaji wa kundi la Udugu wa Kiislamu walikimbilia kujisalimisha wakati wa mapambano hayo siku moja kabla.
Polisi ya Misri imewakamata watu 1004 wanaosadikiwa kuwa ni waungaji mkono wa kundi la Udugu wa Kiislamu katika siku nzima ya mapambano ya nchi nzima jana , imesema wizara ya mambo ya ndani katika taarifa mapema leo Jumamosi(17.08.2013).
Idadi ya waliokamatwa ikiwa ni wafuasi wa kundi la Udugu wa Kiislamu imefikia 1004, taarifa hiyo imesema , mjini Cairo pekee wakiwa wamekamatwa watu 558. Mapambano hayo yamesababisha zaidi ya watu 80 kupoteza maisha, kwa mujibu wa maafisa na watu waliokuwa wakishuhudia katika eneo lililowekwa la muda la kuhifadhi maiti.
Umoja wa Ulaya kujadili ghasia Misri
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamezungumza jana Ijumaa (16.08.2013) juu ya haja ya jibu la pamoja la ghasia nchini Misri na kukubaliana kuitisha mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja huo wiki ijayo.
Rais wa Ufaransa Francois Hollande na kansela wa Ujerumani Angela Merkel wametoa wito wa kumalizwa kwa ghasia na kuanza kwa majadiliano nchini Misri.
Taarifa ya serikali ya Ujerumani imesema kuwa Merkel amemwambia rais wa Ufaransa Hollande kuwa Ujerumani, moja kati ya mshirika mkubwa wa kibiashara na Misri , itaangalia upya uhusiano wake na Misri kuhusiana na umwagaji damu uliotokea wiki hii.
Hollande pia amejadiliana na waziri mkuu wa Italia Enrico Letta na waziri mkuu wa Uingereza David Cameron kuhusu ghasia nchini Misri.
Saudi Arabia wakati huo huo imeeleza kuunga mkono serikali ya mpito nchini Misri inayoungwa mkono na jeshi, ikisema nchi hiyo ya kifalme inaiunga mkono nchi hiyo katika mapambano yake dhidi ya ugaidi na upinzani, ikilenga kuhusu rais aliyeondolewa madarakani Mohammed Mursi wa kundi la Udugu wa Kiislamu.
Maafisa wa Uturuki wameendelea na ukosoaji wao dhidi ya ukandamizaji waandamanaji , wakati rais wa nchi hiyo Abdullah Gul akisema, kile kinachotokea nchini Misri ni aibu kwa Uislamu na mataifa ya Kiarabu. Uturuki na Misri zimewaita nyumbani mabalozi wao kwa ajili ya mashauriano siku ya Alhamis wakati uhusiano wao ukizidi kuharibika.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / dpae / afpe
Mhariri: Caro Robi