1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghasia za kisiasa Misri: Watatu wauawa, mamia wajeruhiwa

3 Februari 2011

Watu watatu wameuawa na wengine kiasi ya 1,500 wamejeruhiwa katika mji mkuu wa Misri Cairo kwenye ghasia za maandamano ya upinzani dhidi ya Rais Hosni Mubarak yanayoingia katika siku yake ya tisa.

Wafuasi wa serikali na wapinzani wakipambanaPicha: AP

Mamia ya wafuasi wa Rais Mubarak na waandamanaji wanaompinga wameendelea kupambana katika eneo la uwanja wa Tahrir.

Wapinzani wanadai kuwa baadhi ya wafuasi hao wa Mubarak ni askari polisi waliyovaa nguo za kiraia.Baadhi yao waliwavamia wapinzani wakiwa na farasi pamoja na ngamia huku wakiwa na silaha kama vile bunduki na visu.

Wafuási wa Mubarak na wapinzani wake wakipambanaPicha: Picture-Alliance/dpa

Taarifa nyengine zinasema wanaume waliovaa miwani nyeusi na wanawake wenye mitindo ya nywele ya gharama na pia wauguzi waliovalia sare nyeupe walionekana upande mmoja wa eneo hilo wakipiga kelele za kumuunga mkono Rais Mubarak.

Wanasiasa wa upinzani wameonya kwamba Misri inaelekea kuingia katika mamlaka ya magenge ya kijambazi. Wanajeshi ambao hadi sasa wamesema hawatojihusisha na upande wowote , walijaribu kufyatua risasi kuwatawanya mahasimu lakini bila mafanikio.

Rais Mubarak hapo siku ya Jumanne alitangaza kwamba hatogombea tena urais,lakini ataendelea kubakia madarakani mpaka uchaguzi mkuu utakapofanyika Septemba mwaka huu.

Mohamed ElBaradei mtu ambaye baadhi wanamchukulia kuwa ni kiongozi wa vuguvugu hilo la umma, amesema siku ya Ijumaa ijayo imepewa jina kuwa ni siku ya kuondoka kwa Rais Mubarak.

UN,UK zatishwa na hali inavyoendelea

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameonya juu ya hatari ya kutokuwepo hali ya utulivu Mashariki ya Kati na kutoa wito kwa pande huko Misri kujizuia.

Katibu Mkuu huyo ambaye alikuwa mjini London kwa mazungumzo na Waziri Mkuu wa Uingerezaa David Cameron ameongezeka kuwa anasikitishwa sana na kuibuka kwa mapigano yasiyokubalika huko Misri.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moonPicha: AP

´´Nasikitishwa sana na kuendelea kwa ghasia na mapigano nchini Misri, kwa mara nyingine tena natoa wito kuzitaka pande zinazohusika kujizuia na ghasia hizo, na kwamba shambulio lolote dhidi ya watu wanaondamana kwa amani ni jambo ambalo halikubaliki´´

Katika mkutano na waandishi pamoja na mwenyeji wake, Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron pia alishutumu ghasia hizo.

Waziri wa Nje wa Ujerumani Guido WesterwellePicha: AP

Mjini Berlin Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle amewaambia waandishi wa habari kwamba muda wa mabadiliko ya kisiasa nchini Misri ni sasa.

Hata hivyo Rais Mubarak amekataa wito wa kumtaka kuondoka haraka madarakani na kuwepo kwa serikali ya mpito kuelekea uchaguzi mkuu.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/ZPR

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW