1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghasia za umwagaji damu zaendelea Ukanda wa Gaza

Daniel Gakuba
13 Novemba 2018

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezitaka Israel na Hamas kujiuzuia, wakati pande hizo zikiendelea na makabiliano ya umwagaji damu katika Ukanda wa Gaza. Uhasama huu umefuatia miezi kadhaa ya utulivu.

Gazastreifen Raketenangriffe
Picha: Getty Images/AFP/M. Kahana

 

Kundi la Hamas limeonya asubuhi ya leo kwamba litaushambulia miji ya Israel ya Beersheba na Ashdod, ikiwa jeshi la Israel litaendelea mashambulizi yake katika Ukanda wa Gaza.

Israel imesema jeshi lake limeyashambulia maeneo zaidi ya 100 ya Hamas katika ukanda huo, ikijibu makombora yapatayo 370 yaliyorushwa na Hamas na kuanguka Kusini mwa Israel kuanzia jana jioni hadi alfajir ya leo.

Ghasia hizi mpya baina ya pande hizo mbili zimefuatia operesheni ya kijasusi ya Israel iliyomuuwa mmoja wa makamanda wa Hamas kilomita kadhaa ndani ya Ukanda wa Gaza juzi Jumapili. Israel imesema operesheni hiyo iliyokwenda vibaya ililenga tu kukusanya taarifa, lakini haikudhamiria kuuwa.

Mtu auawa Kusini mwa Israel

Katika mapigano yaliyofuata, ndege za Israel ziliuwa wanamgambo 7 wa Hamas, huku Hamas ikimuuwa mwanajeshi mmoja wa Israel.Kituo cha televisheni cha Hamas pia kimeshambuliwa, lakini inaripotiwa kuwa wafanyakazi walikuwa tayari wamekimbia.

Basi lililounguzwa na makombora ya Hamas Kusini mwa IsraelPicha: Getty Images/AFP/M. Kahana

Duru za asubuhi ya leo zinaeleza kuwa maiti ya mwanamme mmoja imevutwa kutoka chini ya kifusi cha nyumba iliyoharibiwa na makombora ya Hamas Kusini mwa Israel. Polisi ya Israel ilisema mwanamme huyo alikuwa Mpalestina, na kwamba uchunguzi umeanza kujua sababu ya kuwepo mahali hapo.

Jana, Israel ilisema kombora lililorushwa na Hamas limeharibu bus na kujeruhi abiria wengi. Wakazi wa Ukanda wa Gaza na wa miji ya Kusini mwa Israel wanaelezea hofu ya maisha yao kutokana na ghasia zinazoendelea.

Umoja wa Mataifa wataka pande husika kujizuia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezitaka Israel na Hamas kufanya juhudi kubwa kujizuia, na kulingana na naibu msemaji wa kiongozi huyo, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Nickolay Mladenov anawasiliana kwa karibu na wadau wote, ikiwemo Misri kujaribu kurejesha utulivu.

Makabiliano haya mapya yamekuja baada ya miezi kadhaa ya utulivu kwenye mpaka baina ya Gaza na Israel, ambapo Israel ilikuwa imeiruhusu Qatar kuingiza msaada wa mamilioni ya Dola katika Ukanda wa Gaza, kusaidia malipo ya mshahara kwa wafanyakazi, na kupunguza madhila ya kukatika kwa umeme kwa kila mara.

Baraza la Usalama la Israel ambalo lina mamlaka ya kuanzisha vita lilitarajiwa kukutana asubuhi hii.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe, rtre, ape

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW