1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghasia zapamba moto nchini Tunisia

12 Januari 2011

Machafuko yaliyoanzia Sidi Bouzid nchini Tunisia yameutikisa mji mkuu Tunis jana usiku.Watu 23 wameuwawa tangu machafuko hayo yalipoanza December 16 mwaka jana.Upande wa upinzani unahofia wengi zaidi wamekufa.

Kijana akwepa moshiPicha: picture-alliance/dpa

Vikosi vya usalama vilifyetua risasi hewani na kuvurumisha maguruneti ili kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wakivunja vunja katika kitongoji cha Ettadamen karibu na mji mkuu Tunis.

Kwa mujibu wa ripota wa shirika la habari la Reuters,mamia ya vijana waliwavurumishia mawe polisi kabla ya kuanza kuvunja maduka na kuitia moto benki moja katika eneo hilo.

Wimbi hili jipya la machafuko limeripuka muda mfupi baada ya kuchapishwa ripoti mpya kuhusu idadi ya wahanga wa mashambulio hayo.Ripoti hiyo inasema watu 23 wamefariki badala ya 20 waliotajwa hapo awali.Hata hivyo serikali inakanusha hoja za mashirika ya haki za binaadam yanayodai idadi ya waliouwawa ni kubwa zaidi.

Watunisia wa Ujerumani waandamanaPicha: DW

Souahyr Belhassan wa shirikisho la kimataifa la haki za binaadam,ambalo makao yake makuu yako mjini Paris,amesema waliouwawa ni zaidi ya watu 35 na idadi hiyo inaweza kuwa kubwa zaidi."

Machafuko dhidi ya ughali wa maisha na ukosefu wa ajira hasa miongoni mwa vijana wa Tunisia yamekiuka mpaka wa nchi hiyo ya Afrika kaskazini.Ubalozi wa Tunisia mjini Berne nchini Uswisi umehujumiwa usiku wa jana kuamkia leo.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton ameitolea mwito serikali ya Tunisia " isake ufumbuzi wa amani" kwa mgogoro wa kijamii unaoitikisa nchi hiyo.

Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Al Arabiya mjini Dubai,waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani,Hillary Clinton ameitaka serikali ya Tunisia ijitahidi kubuni nafasi za kazi kwaajili ya vijana.

Picha ya rais Ben Ali juu ya ngome ya HammametPicha: Martina Sabra

Katika hotuba yake kwa taifa jumatatu iliyopita,rais Zine-Al Abidine Ben Ali alisema:

"Tutaitisha meza ya majadiliano- pande zote zinaabidi kushiriki,vyama vya kisiasa,sekta ya kiuchumi,wanazioni na madiwani.Tunataka kiusikiliza wanayosema na kujitahidi kuyapatia ufumbuzi matatizo yao na kuyajua yanayowasumbua."

Machafuko yanayoitikisa Tunisia tangu karibu mwezi mmoja uliopita yamechukua sura ya kisiasa huku upande wa upinzani ukikosoa utawala wa kiimla wa miaka 23 wa rais Zine al Abidine Ben Ali.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters,afp

Mpitiaji:m.Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW