Ghasia zasambaa Paris
8 Februari 2017Magari kadhaa pamoja na shule ya chekechea zimechomwa moto na vijana wakati wa ghasia zilizotokea kati yao na polisi kwenye eneo moja mjini Paris, ambako ghasia za mwaka 2005 zilisababisha ukosoaji mkubwa wa kimataifa kutokana na tofauti iliyopo kati ya mji tajiri wa Paris na vitongoji vinavyouzunguka mji huo.
Kwa mujibu wa polisi, ghasia hizo zilianza kwenye kitongoji cha Aulnay-sous-Bois Februari 2, ambako maafisa wanne wa polisi walishutumiwa kwa kutumia nguvu wakati wakimkamata kijana mwenye umri wa miaka 22, ikiwemo ni pamoja na kumlawiti kwa kutumia kirungu cha polisi, wakati alipotakiwa aonyeshe kitambulisho chake.
Kutokana na ghasia hizo zilizosambaa hadi kwenye miji mitano, polisi wamewakamata watu 17 hadi sasa. Aidha, polisi hao wanne wamesimamishwa kazi, huku mmoja akifanyiwa uchunguzi wa kina na amshafunguliwa mashtaka tangu Jumapili iliyopita, kutokana na tuhuma za ubakaji na wengine watatu kwa tuhuma za vurugu zisizo za lazima na kumshambulia kijana huyo.
Waziri wa mambo ya ndani Ufaransa aonya
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa, Bruno Le Roux amesema serikali inachukua msimamo mkali dhidi ya polisi hao. ''Ninataka kuwakumbusha watumishi wote wa umma katika jeshi la polisi na wale wa vikosi vya ulinzi-Gendarmerie, kuhusu majukumu yao. Najua kwamba kwenye maeneo mengi kuwa visa kama hivi. Sina haja ya kuvitaja, lakini uhusiano kati ya watu na serikali kuu, lazima uzingatiwe katika taifa letu,'' alisema Le Roux.
Kijana huyo aliyetajwa kwa jina moja tu la Theo, ametoa wito wa kuwepo utulivu na familia yake imesema inauamini mfumo wa haki na sheria nchini Ufaransa na wanatarajia kesi hiyo itasikilizwa kwa kuzingatia haki. Jana jioni Rais wa Ufaransa, Francois Hollande alimtembelea kijana huyo aliyelazwa hospitali ambako anatibiwa tangu alipofanyiwa udhalilishaji huo.
Wakati hayo yakijiri inaarifiwa kuwa mgombea wa urais kupitia chama cha kihafidhina nchini humo, Francois Fillon leo amewatolea wito wapiga kura waendelee kumuunga mkono, baada ya kupoteza nafasi yake kama mgombea anayeongoza kutokana na tuhuma za kuwalipa mishahara watu wa familia yake kwa kazi ambazo hawajawahi kuzifanya.
Kashfa hiyo imemlazimisha Fillon kuomba radhi na kiwango cha umaarufu wake kimeshuka. Utafiti wa maoni ya wapiga kura unaonyesha kuwa mgombea wa kujitegemea mwenye kufuata siasa za mrengo wa wastani, Emmanuel Macron kama anayeweza kushinda katika uchaguzi wa mwezi Aprili na Mei, na kumshinda kiongozi wa chama cha National Front kinachofuata siasa kali za mrengo wa kulia, Marine Le Pen katika duru ya pili ya uchaguzi kwa theluthi mbili ya kura.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP, Reuters
Mhariri: Saumu Yusuf