Ghasia zimepungua Ufaransa
2 Julai 2023Mauaji ya kijana huyo yamesababisha kuibuka kwa machafuko kote Ufaransa ambapo takribani polisi 45,000 wamesambazwa kuyakabili.
Kulingana na taarifa ya wizara ya mambo ya ndani ya nchi hiyo zaidi ya watu 700 walikamatwa Jumamosi usiku ikilinganishwa na 1,311 waliokamatwa usiku wa Ijumaa. Awali, Alhamisi usiku, watu 875 nao walikamatwa kutokana na vurugu hizo.
Katika vurumai hizo, waandamanaji wamechoma magari, usafiri wa umma na wamepora maduka. Waandamanaji hao pia walilenga majengo ya halmashauri za miji, vituo vya polisi na shule na majengo yanayowakilisha taifa la Ufaransa. Ghasia zaidi zilizofanyika usiku zimeshuhudiwa katika mji wa Marseille ambako polisi walitumia mabomu ya machozi kupambana na kuwatawanya vijana katikati ya mji.
Makazi ya Meya yashambuliwa
Licha ya ripoti za kupungua kwa machafuko Ufaransa, waandamani ambao wengi wao ni vijana wadogo wamepambana na polisi leo asubuhi wakilenga nyumba ya Meya wa kitongoji cha l'Hay-les-Roses jijini Paris kwa kutumia gari linalowaka moto.
Meya huyo, Vincent Jeanburn amesema mke wake na mmoja kati ya watoto wake walijeruhiwa katika tukio hilo lililojiri saa 1:30 usiku wakati wakiwa wamelala. Jeanburn amesema wakati huo alikuwa kwenye ukumbi wa halmashauri ya mji akifuatilia ghasia zilizokuwa zikiendelea.
Jeanburn ambaye ni mwanachama wa chama cha upinzani cha kihafidhina cha Republican katika taarifa yake amesema, shambulio hilo linawakilisha "hofu na aibu" kwenye fujo hizo, na serikali inapaswa kutangaza hali ya hatari.
Soma zaidi: Hamkani bado si shwari Ufaransa kufuatia kifo cha Nahel
Kutokana na vurugu hizo, China na mataifa ya magharibi yamewatahadharisha raia wake kuwa makini na machafuko ambayo yanaweza kusababisha changamoto kubwa kwa Ufaransa, wakati wa msimu wa kilele cha majira ya kiangazi ambao huwa na watalii wengi hasa katikati ya miji.
Jumapili, ofisi ya ubalozi mdogo wa China iliarifu kuwa, ubalozi huo umewasilisha malalamiko rasmi kwa Ufaransa baada ya basi lililokuwa limebeba kundi la watalii wa China kuvunjiwa viyoo mapema Alhamisi. Tukio hilo liliwasababishia watalii hao majeraha madogo madogo.
Iran yaitaka Ufaransa iache unyanyasaji kwa watu wake
Katika hatua nyingine, Iran hii leo imeitolea wito Ufaransa wa "kukomesha unyanyasaji kwa raia wake" kutokana na wimbi la machafuko yaliyosababishwa na kitendo cha polisi kumuua kijana Nahel M. tukio lililotokea Jumanne wiki iliyopita. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa Iran Nasser Kanani alitoa wito huo kupitia mtandao wa Twitter na kuwataka raia wake waepuke safari zisizo za lazima kuelekea Ufaransa.
Machafuko ya Ufaransa yamegonga vichwa kwenye magazeti ya Iran ambayo nayo ilikumbwa na maandamano yaliyofanyika kote nchini humo mwaka uliopita yaliyochochewa na kifo cha mwanamke mwenye umri wa miaka 22 mwenye asili ya Kikurdi Mahsa Amini akiwa mikononi mwa polisi kwa madai ya kukiuka sheria kali za mavazi ya wanawake nchini humo.