1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kamanda Haftar ahimizwa kusitisha mashambulizi Tripoli

17 Aprili 2019

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Libya Ghassan Salame ametaka kusitishwa kwa mashambulizi yanayofanywa katika mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli

LNA Chef Khalifa Haftar
Picha: picture-alliance/ Balkis Press

Katika ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, Salame amesema na hapa naunuku ujumbe wake, "Usiku mbaya kabisa wa kushambuliwa ghafla kwa maeneo ya makaazi ya watu.

Mashambulizi haya yasitishwe mara moja kwa ajili ya raia milioni tatu wanaoishi katika Mji Mkuu wa Tripoli," mwisho wa kunukuu.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Libya Ghassan SalamePicha: picture-alliance/AP Photo/Thein Zaw

Msemaji wa wizara ya afya Malek Merset amesema leo kuwa karibu watu 26 wamejeruhiwa pia katika mashambulizi ya roketi ya usiku kucha katika wilaya ya Abu Salim.

Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa WHO nalo linasema watu 189 wameuwawa katika wiki mbili za mapigano huko Tripoli.

Makundi hasimu ambayo yamehusika katika mapigano yamelaumiana kwa mashambulizi hayo. Kamanda Khalifa Haftar na vikosi vyake wamesema mashambulizi yanayofanywa na upande wake ni sehemu ya kampeni ya kuleta amani na kuwashinda waliowataja kuwa ''magaidi'' katika nchi hiyo iliyokumbwa na machafuko tangu kupinduliwa kwa utawala wa kiimla wa Muammar Gaddafi mwaka 2011.

Khalifa Haftar aonekana kama mtu hatari na dikteta

Lakini serikali ya Libya inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Serraj na ambayo inatambulika kimataifa, inamuona jenerali Haftar mwenye umri wa miaka 75 kama mtu hatari ambaye atakuwa dikteta. Fathi Bashagha ni waziri wa usalama wa ndani katika serikali hiyo ya mjini Tripoli.

"Huu ni ugaidi na huyu kamanda Haftar ni mtu mwendawazimu. Ni mambo ya kushangaza sana, huezi kuamini kwamba anaweza kuwauwa watu wake namna hii, kuishambulia Tripoli kwa maguruneti. Na unajua kuna kiasi kikubwa cha watu hapa, zaidi ya watu milioni 3," alisema Fathi Bashagha 

Baadhi ya vikosi vya Kamanda Halifa HaftarPicha: Reuters/E. O. Al-Fetori

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu msaada wa kibinadamu, OCHA katika taarifa limesema maelfu ya watu wamekwama katika wilaya za kusini mwa Tripoli kutokana na mapigano hayo. Waokoaji na wafanyakazi wa kutoa misaada wamekuwa na wakati mgumu kuwafikia wanaohitaji usaidizi, na huduma za umeme, maji na mawasiliano zimetatizwa kwa kiasi kikubwa.

Hakuna maelewano ya pamoja yaliyotangazwa na mataifa yenye nguvu duniani kutokana na misimamo tofauti ya nchi za Ghuba na Ulaya kuelekea pande mbili zinazozozana.

Waziri Mkuu wa Italia Matteo Salvini amesema mashambulizi yanayofanywa na vikosi vya Haftar yameongeza uwezekano wa wanamgambo kuingiza boti za wahamiaji nchini mwake.

Italia ambayo kimaslahi inayataka mafuta ya Libya, inamuunga mkono Serraj, hatua ambayo inaleta mkwaruzano na Ufaransa ambayo inamuunga mkono Haftar.