1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Giuseppe Conte akubali kuunda serikali mpya Italia

29 Agosti 2019

Giuseppe Conte ameahidi kuunda serikali na kutaja majina ya mawaziri katika siku chache zijazo. Hata hivyo wachambuzi wa siasa wana mashaka ikiwa serikali hiyo itadumu kufuatia tofauti za kisiasa kati ya vyama husika.

Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte akiwasili katika ikulu ya rais Sergio Mattarella kwa mkutano.
Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte akiwasili katika ikulu ya rais Sergio Mattarella kwa mkutano.Picha: Reuters/Presidential Palace/F. Ammendola

Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte amesema amekubali jukumu ambalo amepewa na rais Sergio Mattarella leo la kuunda serikali mpya. Aidha amesema anatumai atakuwa na orodha ya mawaziri katika siku chache zijazo. 

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupata agizo kutoka kwa Rais Sergio Mattarella la kuunda serikali mpya, Giuseppe Conte amesema serikali mpya itahitajika kuifanyia kazi mara moja bajeti na kuepusha kitisho cha ongezeko la kodi za mauzo.

Conte alijiuzulu wiki iliyopita baada ya chama cha siasa kali za mrengo wa kulia The League kujiondoa kwenye muungano wa serikali uliojumuisha pia vuguvugu la Nyota 5. Hata hivyo Chama cha vuguvugu la nyota tano M5S na chama cha Democratic PD waliokuwa mahasimu wakubwa hapo jana walikubali kuungana na kuunda serikali kufuatia kuanguka kwa serikali ya siasa za kizalendo mapema mwezi huu.

Conte amesema atarudi kwa rais katika siku chache zijazo kuwasilisha pendekezo lake la mawaziri. Ameongeza pia kusema kuwa:

"Huu ni wakati wa msimu mpya. Msimu muhimu wa mageuzi, uzinduzi na matumaini. Msimu unaotoa majibu na uhakikisho kwa nchi yetu."

Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude JunkerPicha: Picture alliance/dpa/epa/Y. Valat

Junker amtakia Conte mafanikio

Hayo yakijiri, rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Junker amemtakia Giuseppe Conte mafanikio katika juhudi zake za kuunda serikali mpya

Msemaji wa halmashauri hiyo Mina Andreeva amesema Italia ni mshirika muhimu katika Umoja wa Ulaya na wanaitegemea katika miradi ya Ulaya. Ameongeza kuwa Junker atakuwa na mawasiliano na Conte baadaye leo.

Masoko ya hisa yameikaribisha hatua hiyo ambayo imemaliza wiki tatu za mkwamo wa kisiasa uliosababishwa na kiongozi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Matteo Salvini aliyekiondoa chama chake katika serikali ya mseto baada ya wiki kadhaa za mizozano ya hadharani.

Hata hivyo bado vuguvugu la nyota tano pamoja na chama cha PD vitahitaji kukubaliana kuhusu sera ya pamoja na pia orodha ya mawaziri. Lakini mkuu wa vuguvugu la nyota tano Luigi Di Maio na mwenzake wa PD Nicola Zingaretti wamesema wameahidi kuelewana kwa masilahi ya taifa.

Kiongozi wa vuguvugu la M5S, Luigi Di MaioPicha: Getty Images/AFP/T. Fabi

Wachambuzi wa siasa na baadhi ya raia Italia watilia mashaka ikiwa serikali mpya itadumu

Kiongozi wa chama cha M5S Luigi Di Maio amesema makubaliano kati ya chama hicho na chama cha PD ni lazima yaidhinishwe na wanachama wa chama chake katika kura ya mtaondoni inayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa juma.

Hata hivyo wachambuzi wa siasa wameonya kuwa makubaliano na vuguvugu la nyota tano ambalo lilishaapa kutoshirikiana na vyama vya zamani; na kile cha mrengo wa wastani kushoto, huenda yakavunjika mapema.

Baadhi ya Waitaliano waliozungumza na shirika la habari la Reuters, pia walikuwa na hisia mseto. Wapo walioelezea matumaini finyu ya serikali mpya itakayoundwa kudumu wakitaja tofauti kubwa zilizoko kisiasa kati ya vyama husika.

Aidha wapo wanaohisi kupata ahueni na kutumai itatoa suluhisho la haraka kwa matatizo ya nchi hiyo ya tatu kiuchumi katika Umoja wa Ulaya.

Vyanzo: RTRE, DPAE,AFPE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW