Gloria Orimba na juhudi za kukuza ajira kwa vijana
1 Desemba 2025
Mbali na yote hayo, kuna taka pia za plastiki ambazo wengi hudhani kuwa hazina thamani. Hata hivyo, hali ni tofauti kwa Gloria Orimba, mmoja wa waanzilishi wa kikundi cha wakusanyaji taka hapa Kisumu nchini Kenya. Gloria, ni Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Clean Kisumu, akiwa mwanamke aliyethubutu kuwekeza muda wake na rasilimali katika sekta hii.
Takriban kilomita 3 kutoka katikati mwa Kisumu mjini ni eneo la kukusanya taka ambako ni makao makuu ya kampuni ya Clean Kisumu inayopatikana eneo linalofahamika kama "ghorofa chafu".
Taka hutengwa kulingana na vitengo maalum
Hapo shuguli ni nyingi, na endapo wewe ni mgeni, taswira ya kwanza, utadhani eneo hili ni jaa la taka, ila mambo ni tofauti unapoingia ndani, kuanzia langoni utakutana na mikokoteni ya kusafirisha taka iliyoegeshwa, sehemu ya kupimia taka za plastiki, chupa, na kadhalika, yaani ni sehemu iliyojaa shuguli nyingi.
Gloria Orimba anasema kila mmoja hapo anawahi kutekeleza majukumu yake, katika eneo hilo lenye takriban robo ekari. Takataka hugawanywa kulingana na vitengo, wapo wanaopasua chupa na kuzisaga na wengine wanashughulika na taka za plastiki, wapo wanaoondoa makaratasi yaliyobandikwa kabla ya kukusanya taka hizo katika makumi ya tani zinazonunuliwa na kampuni za kutengeneza bidhaa mbalimbali kutokana na rasilimali hii.
''Tunakusanya takataka kutoka majumbani, kwenye migahawa, maduka ya jumla, sehemu za burudani na wapo pia wanaotuletea plastiki na chupa. Taka za kuoza tunazisafirisha hadi eneo kuu la kutupia taka Kisumu ambalo ni Kasese. Tunachakata taka zilizosalia tukitofautisha za plastiki, karatasi, chupa na kadhalika,'' alisisitiza Gloria.
Pesa za wateja wanaochukuliwa takataka kutoka kwenye maeneo yao ndio chanzo cha mapato yanayotumiwa kuwalipa watu wanaohudumu kwenye kampuni hiyo. Gloria anasema malengo ya kuanzishwa kwa kampuni yalichangiwa na ari ya kujikimu kimaisha.
Washirika katika kuyatunza mazingira
Lakini yeye na washirika wake hawakutarajia hatua hii ingebadilisha maisha ya wengine wengi na baadae kuwaelekeza katika harakati za kuyalinda na kuyatetea mazingira.
Kulingana na Afisa Mkuu Mtendaji huyo wa kampuni ya Clean Kisumu, watu wanapomaliza shule na harakati za kutafuta kazi inaishia kuwa kazi tena. Aidha, Gloria anasema alipokuwa na wenzake enzi za ujana wao, waliamua waanze kukusanya taka na kujipatia pesa kidogo,
''Kadri muda ulivyozidi tukapata washirika wengine na tukaendelea kijiimarisha. Kuhusu harufu, hii kazi inataka moyo ila tunatumia baadhi ya vifaa kujiweka salama.Pia tunatambua ni katika harufu hii tumebadilisha maisha ya wengi,'' alibainisha Gloria.
Makundi kadhaa ya vijana wakiwemo waliobadilisha tabia ya vijana wa kurandaranda mitaani na uraibu wa mihadarati, sasa wamepata dira mpya na kujikwamua kimaisha kutokana na ajira hiyo inayotokana na kuchakata taka. Octojaz Odhiambo anasema awali maisha yake yalikuwa tu mitaani lakini kupitia uwekezaji huo ameona mabadiliko.
''Nilikuwa navuta guluu, kula ilikuwa shida, nikibahatika ni chakula cha kwenye takataka. Sikuwahi jua kwamba maisha yangu yanaweza kubadilika, na sasa naweza hata kulipa kodi ya nyumba yangu, alifafanua Odhiambo.
Kuridhika kwa wafanyakazi
Kwa upande wake Edwin Omondi anasema anafurahi kufanya kazi na Gloria, kwani sasa anaishi vizuri na familia yake. ''Sasa niko sawa kabisa. Ninaishi salama na familia yangu. Gloria hana shida na mtu na anatusaidia tunafanya kazi vizuri kabisa,'' alisema Omondi.
Ni kutokana na juhudi za pamoja, Gloria na kundi lake wamepata ufanisi. Wengi wanampongeza kama kielelezo cha kuwa mwanamke aliyevunja vikwazo vya upatikanaji wa ajira kupitia katika kuyalinda mazingira. Mike Wanjeng'u ambaye ni mshirika wa Gloria, akihudumu kama Mkurugenzi wa Ushirikiano anasema, anajivunia ushirikiano uliopo akisisitiza kuwa, ili kuyaokoa mazingira na kuchangia katika juhudi za kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kwani kila mmoja anastahili kutekeleza wajibu wake na kwamba mafanikio makubwa yanaanzia nyumbani.