GMO yatishia kumuondosha waziri Kenya
22 Novemba 2022Kwenye taarifa yao ya pamoja, wabunge wa eneo la kaskazini mwa Bonde la Ufa - ambalo lina utajiri mkubwa wa kilimo cha mahindi - walitishia kumvua madaraka Waziri wa Viwanda Moses Kuria aliyeamuru mahindi kuagizwa kutokea nje.
Wakiongozwa na Seneta wa Nandi, Samson Cherargei, walishinikiza siku ya Jumanne (Novemba 22) mchakato huo usitishwe haraka iwezekanavyo.
Kwa upande wake, mbunge wa Pokot Kusini, David Pkosing, aliweka bayana kuwa wangelikusanya saini kuanzia Jumatano (Novemba 23), lengo likiwa ni kumvua madaraka waziri huyo wa viwanda.
Wabunge hao walihoji chanzo cha meli iliyosheheni mahindi kutokea nje kufunga gati mjini Mombasa pasina kufuata muongozo wa sheria, wakati bado notisi ya Gazeti Rasmi la Serikali ya kuagiza mahindi kutoka nje iilikuwa inasubiriwa.
Taarifa ya Mamlaka ya Bandari nchini Kenya (KPA) iliyochapishwa siku ya Jumanne ilielezea kuwa meli 37 zinatazamiwa kutia nanga bandarini Mombasa.
Ya nne kwenye orodha hiyo ni meli kwa jina Africa Merlin iliyosheheni magunia yasiyopungua 200,000 yenye nafaka na mengine matupu iliyoripotiwa kuwasili siku hiyo ya Jumanne.
Wabunge hao waliungwa mkono kwenye madai hayo na wenzao wa eneo la magharibi ya Kenya ambao walisema "kitendo hicho cha kuagiza mahindi kutoka nje hakitaleta tija."
Mjadala wa GMO kupambana na njaa
Wakati huo huo, kwenye mjadala wa bunge la Kenya siku ya Jumanne (Novemba 22) wabunge waliwasilisha hoja zao kupinga na kuunga mkono suala la kuagiza mahindi kutoka nje.
Kiongozi wa chama tawala bungeni, Kimani Ichungwa - aliye pia mbunge wa Kikuyu - alishikilia kuwa "wakulima wana wajibu wa kufanya la sawa ndipo soko lisawazishwe."
Wiki iliyopita, Kuria alitangaza kuwa serikali ya Kenya ilipitisha uamuzi wa kuridhia magunia milioni 10 ya mahindi yaliyobadilishwa vinasaba kuagizwa pasina kutozwa kodi katika muda wa miezi sita ijayo.
Kauli hizo zimezua hisia mseto nje ya serikali kuu. Kiongozi wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga, alisisitiza kuwa "wakulima ndio watakaoumia."
Itakumbukwa kuwa Raila Odinga alipokuwa waziri mkuu aliunga mkono kitendo cha kuagiza na kutumia vyakula vilivyobadilishwa maumbile ya vinasaba(GMO).
Imeandikwa na Thelma Mwadzaya/DW Nairobi