Gnabry arefusha mkataba wake na Bayern hadi 2028
6 Februari 2026
Winga wa klabu ya Bayern Munich Serge Gnabry ameongeza mkataba wake hadi mwaka 2028. Gnabry mwenye umri wa miaka 30, alijiunga na miamba hao wa Bavaria tangu mwaka 2017 baada ya kupita katika vikosi kadhaa ikiwemo Arsenal, West Brom na Werder Bremen.
Mkataba wa Gnabryulikuwa unamalizika majira ya kiangazi. Winga huyo ameshinda ubingwa mara sita wa ligi ya kandanda ya Ujerumani Bundesliga akiwa na Bayern sambamba na Ligi ya Mabingwa Ulaya, Champions League.
Baada ya tetesi za kuondoka, msimu huu ameonesha kiwango bora kwa mabao sita na asisti tano katika mechi 15 za Bundesliga.
Akiwa na mabao 100 na asisti 69 katika mechi 311, Gnabry ameimarisha nafasi yake kama moja ya nguzo muhimu za Bayern, akiunda ushirikiano hatari na Harry Kane pamoja na winga Michael Olise na Luis Díaz.
Akiweka wazi sababu za kusaini upya mkataba, alisema anajihisi "nyumbani kabisa” Munich; kuanzia timu, makocha, mashabiki hadi mazingira ya jiji. Aliongeza kwamba anaona kuna kikosi bora kinachoweza kufanya makubwa, na kwamba hakudhani kama angedumu hapo miaka 10.
Mkurugenzi wa michezo Max Eberl amemtaja Gnabry kama "nguzo muhimu” na mfano wa kuigwa, huku mchezaji huyo pia akirejea kuwa sehemu muhimu ya timu ya taifa ya Ujerumani chini ya Julian Nagelsmann.