Gnassingbé, mpatanishi mpya wa Rwanda na Kongo
15 Aprili 2025
Rais wa Togo Faure Gnassingbé ana uzoefu katika upatanishi. Bila shaka aliwezesha kuachiliwa nchini Mali, mnamo Januari 2023, kwa wanajeshi 46 wa Ivory Coast wanaoshukiwa kuwa mamluki.
Lakini kuhusu mzozo kati ya Kinshasa naKigali, sasa rais huyo wa Togo anarithi mgogoro tata zaidi. Kwa hiyo mashaka yanaendelea kuhusu uwezo wa rais wa Togo kufikia kile ambacho mwenzake wa Angola, Joao Lourenço, alishindwa kukifikia kwa miaka mitatu.
Lourenco ndiye aliyependekeza jina la Gnassingbé
Hata hivyo, Lourenco ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika, ndiye alipendekeza jina la Faure Gnassingbé kumrithi. Mwezi Machi uliopita, kufuatia mpango ambao haukutarajiwa wa Qatar na mkutano wa marais wana Rwanda huko Doha, rais wa Angola alitangaza kuwa anasitisha upatanishi wake katika mzozo wa mashariki mwa Kongo.
Wajumbe wa M23 na serikali ya Kongo wakosa kukubaliana kuhusu mambo fulani Doha
Faure Gnassingbé anachukua jukumu lake wakati wajumbe wa M23 na serikali ya Kongo wako Doha, bila kufanikiwa kukubaliana juu ya mambo fulani. Uasi huo unaripotiwa kudai hatua za kujenga imani, na kwa upande wake, inataka kusitishwa kwa mapigano bila masharti na kuondolewa kwa waasi katika miji inayokaliwa kimabavu.
Ingawa Rais wa Qatar, Tamim bin Hamad al-Thani, aliweza kuwaleta pamoja marais wa Rwanda na Kongo, Wakongo wengi hawakufurahia upatanishi huu usio wa Kiafrika.
Kagame: Tutalinda usalama wa Rwanda kwa gharama yoyote
Mkuu wa nchi wa Togo pia anajiunga na upatanishi mwingine wa hivi karibuni, ule wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kundi la watu watatu linalojumuisha Olusegun Obasanjo, rais wa zamani wa Nigeria, Uhuru Kenyatta, rais wa zamani wa Kenya na Catherine Samba Panza, rais wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Waasi waM23, wanaoungwa mkono na Rwanda, walifanya mashambulizi makubwa mwishoni mwa Januari na kuteka miji miwili mikubwa mashariki mwa Kongo, Goma na Bukavu, ndani ya wiki chache.
Tangu wakati huo, wito kutoka kwa jumuiya ya kimataifa wa kutaka kundi hilo na wanajeshi wa Rwanda waondoke haujatekelezwa. Mwanzoni mwa Aprili, waasi waM23 walitangaza kujiondoa kutoka mji wa Walikale, sambamba na ziara mjini Kinshasa ya mshauri maalum wa rais wa Marekani Donald Trump kwa Afrika, Massad Boulos.
Gnassingbé, pia anajaribu kuzirejesha Mali, Niger na Burkina Faso katika Jumuiya ya ECOWAS
Faure Gnassingbé, ambaye pia anajaribu kuzirejesha Mali, Niger na Burkina Faso katika Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi, kwanza atalazimika kujipa nafasi zaidi pamoja na wapatanishi wengine wawili, akiwemo yule mwenye ushawishi mkubwa kutoka Qatar.
Lakini hata hivyo, Robert Dussey, waziri wa mambo ya nje wa Togo alisema kuwa mpatanishi mpya wa mzozo wa Kongo atachangia kikamilifu katika kutafuta amani ya kudumu, maridhiano na utulivu katika eneo la Maziwa Makuu.