1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Grace Mugabe apata kinga na kurejea Zimbabwe

20 Agosti 2017

Baada ya kupewa kinga ya kidiplomasia na serikali ya Afrika Kusini, mke wa rais wa Zimbabwe Grace Mugabe alirejea nyumbani siku ya Jumapili, licha ya miito kwamba ashitakiwe kwa madai ya kumshabulia mwanamitindo Jo'berg.

Simbabwe Grace Mugabe Präsidentingattin
Picha: Getty Images/AFP/J. Njikizana

Shirika la utangazaji la Zimbabwe ZBC lilimuonyesha Grace Mugabe akisalimiana na maafisa wa serikali na jeshi katika uwanja wa ndege wa Harare baada ya kushuka kwenye ndege ya shirika la ndege la Zimbabwe pamoja na mume wake, ambaye alihudhuria mkutano wa kilele wa viongozi wa kanda ya kusini mwa Afrika mjini Pretoria. Mugabe na mke wake hawakuhudhuria mazishi ya kitaifa ya afisa mwandamizi wa chama tawala katika mji mkuu wa Zimbabwe; kawaida rais anakuwa mgeni rasmi katika matukio kama hayo.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Afrika Kusini, Maite Nkoana-Mashabane, ilimpa kinga ya kidiplomasia Grace Mugabe kupitia taarifa iliyochapishwa katika gazeti la serikali lililochapishwa siku ya Jumapili. Taarifa hiyo iliyosainiwa siku ya Jumamosi, inatambua "kinga na fursa za mke wa rais wa Zimbabwe, Dk. Grace Mugabe."

Awali polisi ya Afrika Kusini ilitoa tahadhari ya kiusalama kwenye maeneo ya mipakani kuhakikisha haondoki bila kutambuliwa, na walisema walikuwa wanasubiri uamuzi wa serikali kuhusu maombi ya kinga.

Mwanamitindo Gabriella Engels akionyesha jeraha alilolipata baada ya kupigwa kwa waya na mke wa rais wa Zimbabwe, Grace Mugabe.Picha: picture-alliance/dpa/AP/Debbie Engels

Chama kikuu cha upinzani nchini humo, cha Democratic Alliance kimetaka ufanyike uchunguzi wa bunge kuhusu uamuzi wa serikali kumuachia mke wa rais wa Zimbabwe kuondoka na kilisema kupitia ukurasa wake wa twitter, kwamba serikali haikuwa tena na uhalali katika nyanja ya diplomasia ya kimataifa na inaonyesha kupuuza kabisaa utawala wa sheria.

Kisa chalinganishwa na kuachiwa Hassan al-Bashir 2015

John Steenhuisen, afisa mwandamizi wa upinzani, alilinganisha namna serikali ya Afrika Kusini ilivyoshughulikia kesi ya Mugabe na uamuzi wa serikali kumruhusu Rais wa Sudan Omar al-Bashir kuondoka nchini humo mwaka 2015, hata wakati alipotakiwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu kwa madai ya uhalifu wa kivita, liliripoti shirika la Afrika.

Gabriella Engels, mwanamitindo mwenye umri wa miaka 20, alisema Grace Mugabe alimshambulia Agosti 13, kwa kumchapa na waya wa umeme uliomkata kwenye paji la uso. Likizungumzia habari za kurejea kwa Mugabe nchini Zimbabwe, kundi linalomwakilisha Engels lilisema Jumapili kwamba litakwenda mahakamani kuipinga serikali ya Afrika Kusini kuhusu suala la kinga.

"Tutatumia mkakati wa muda mrefu kuhusu suala hili," alisema Willie Spies, mwakilishi wa kisheria kutoka kampuni ya AfriForum, ambalo ni shirika linalowawakilisha Waafrika Kusini weupe wa jamii ya wachache ya Afrikaner.

"Anaweza kuwa amerudi Zimbabwe, lakini hiyo inaweza kumaanisha kwamba itakuwa vigumu kwake kuja tena Afrika Kusini huko mbeleni," Spies alisema. Vyombo vya habari vya serikali ya Zimbabwe vimekuwa kimya kwa kiasi kikubwa kuhusu kadhia hiyo ya mke wa rais wa Zimbabwe.

Mke huyo wa rais wa Zimbabwe amekosolewa kwa kuwa na hasira za haraka na safari za manunuzi makubwa, lakini nyota yake ya kisiasa inayozidi kupanda imewafanya baadhi wajiulize iwapo anafanya mikakati ya kumrithi mume wake.

Grace na mume wake Rais Robert Mugabe.Picha: Getty Images/AFP/J. Njikizana

Hivi karibuni alisema chama tawala cha Zimbabwe kinapaswa kurejesha kipengee kwenye katiba, kinachosema kwamba mmoja wa makamu wa rais anapaswa kuwa mwanamke, alimpa changamoto waziwazi mume wake mwenye umri wa miaka 93 atangaze mrithi.

Pia siku ya Jumapili, mmoja wa makamu wawili wa rais wa Zimbabwe, Phelekezela Mphoko, aliongoza mazishi ya Shuvai Ben Mahofa, mwanachama mwandamizi wa chama tawala cha Zanu-PF aliefariki wiki moja iliyopita.

Kuzuwiliana safari za ndege za mashirika ya serikali

Shirika la ndege la Afrika Kusini wakati huo lilisema Jumapili - saa chache baada ya Mugabe kurejea mjini Harare - kwamba lilikuwa linarejesha safari zake kati ya Afrika Kusini na Zimbabwe, baada ya safari hizo kuzuwiwa na maafisa wa Zimbabwe.

Hatua ya Zimbabwe iliochukuliwa Jumamosi, ilifuatia kuzuwiwa kwa ndege ya shirika la Zimbabwe katika uwanja mkuu wa Johannesburg Ijumaa jioni. Ndege hiyo iliruhusiwa kuruka Jumamosi usiku, walisema maafisa wa usafiri wa anga. HAikuwa bayana iwapo Mugabe alitumia ndege hiyo hiyo kurejea nchini Zimbabwe.

Mataifa yote mawili yalisema yameweka vikwazo kwa sababu ndege zilizoathiriwa hazikuwa na vibali vya operesheni za nje." Willie Spies, wakili anaemwakilisha mwanamitindo aliesema ameshambuliwa, alisema huenda mgogoro huo wa safari za ndege ulikuwa njama iliyosanifiwa kuondoa nadhari kutoka kwenye matatizo ya mke wa rais.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape

Mhariri: Lilian Motono.