Greenland: Denmark na Marekani kwenye meza ya majadiliano
14 Januari 2026
Mvutano wa kidiplomasia kuhusu mustakabali wa Greenland unaendelea kuchukua sura mpya, huku mazungumzo ya ngazi za juu yakipangwa kati ya Denmark na Marekani. Waziri wa Mambo ya Nje wa Denmark, Lars Løkke Rasmussen, anatarajiwa kufanya mazungumzo nyeti mjini Washington na Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio.
Mazungumzo haya yanahusu madai ya Marekani juu ya Greenland, eneo lenye umuhimu mkubwa wa kimkakati katika Aktiki, hasa kwa masuala ya usalama na rasilimali.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Greenland, Vivian Motzfeldt, pia anatarajiwa kuhudhuria mkutano huo. Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen, amesema ushiriki wa Makamu wa Rais Vance ulikuwa uamuzi wa dakika za mwisho, akieleza kuwa awali mkutano huo ulikuwa umepangwa katika ngazi ya mawaziri wa mambo ya nje pekee.
Frederiksen, pamoja na Waziri Mkuu wa Greenland, Jens-Frederik Nielsen, wameweka wazi msimamo wao kuwa Greenland haiuzwi na haiwezi kuunganishwa na Marekani. Frederiksen amekiri kuwa si rahisi kustahimili kile alichokiita shinikizo lisilokubalika kutoka kwa washirika wa karibu, akionya kuwa kipindi kigumu zaidi bado hakijafika.
Akizungumzia hali hiyo, Mbunge wa Bunge la Greenland, Juno Berthelsen, amesema wananchi wa Greenland wana wawakilishi wao halali na wamekuwa wakisisitiza diplomasia tangu mwanzo.
"Wananchi wa Greenland wana wawakilishi wao na wanasiasa wao. Tangu mwanzo tumekuwa tukitaka mazungumzo ya kidiplomasia ili kutafuta suluhu. Tunafurahia kuona juhudi hizo sasa zikifanyika. Kwa zaidi ya mwaka mmoja kumekuwa na maneno mengi kutoka pande zote, lakini tulichohitaji ni mazungumzo ya kweli kuhusu hali ilivyo na mahusiano kati ya Marekani na Greenland, Greenland na Denmark, pamoja na Marekani na Denmark."
Katika mazungumzo yanayotarajiwa Washington, Denmark inapendekeza kuimarisha ushirikiano wa kiusalama katika eneo la Aktiki kupitia NATO, kwa kushirikiana na washirika wa Ulaya, ikisisitiza kuwa inalenga kubaki mshirika mwaminifu wa muda mrefu wa Marekani bila kuhatarisha uhuru wa Greenland.
Athari kwa NATO na usalama wa Ulaya
Wakati huo huo, wabunge wa Marekani wamewasilisha muswada wa pande mbili unaolenga kuzuia serikali ya Rais Donald Trump kuchukua, kuikalia au kudhibiti eneo la nchi mwanachama wa NATO bila ridhaa ya taifa husika.
Muswada huo umeungwa mkono na Seneta Lisa Murkowski na Seneta Jeanne Shaheen, wakionya kuwa jaribio lolote la kuitwaa Greenland litakiuka mkataba wa NATO na kudhoofisha mshikamano wa muungano huo, hasa katika kukabiliana na vitisho kutoka Urusi na China.
Katika hatua nyingine ya wazi ya kisiasa, Ufaransa imetangaza kuwa itafungua ubalozi mdogo Greenland tarehe 6 Februari.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noël Barrot, amesema hatua hiyo ni ishara ya kisiasa inayolenga kuonyesha mshikamano na uwepo mpana wa Ulaya katika kisiwa cha Greenland, ikijumuisha nyanja za kisayansi. Uamuzi huo ulifikiwa katika msimu wa kiangazi kufuatia ziara ya Rais Emmanuel Macron huko Greenland.
Greenland imeendelea kusisitiza kuwa imechagua kubaki eneo linalojitawala chini ya Denmark, ndani ya mfumo wa NATO na ushirikiano wa Ulaya. Ingawa Rais Trump amedai kuwa Marekani inaihitaji Greenland kwa sababu za kiusalama, rasilimali za madini na hofu ya ushawishi wa Urusi na China katika eneo la Aktiki, viongozi wa Greenland na Denmark wanasisitiza kuwa mustakabali wa kisiwa hicho utaamuliwa na watu wa Greenland wenyewe — kupitia diplomasia, si shinikizo.