Greenpeace yahimiza moto wa Bonde la Kongo ushughulikiwe
28 Agosti 2019Shirika la kimataifa la ulinzi wa mazingira Greenpeace limezitaka serikali za mataifa yaliyo katika Bonde la Kongo kuchukua hatua zaidi kupambana na moto wa msitu wa Afrika ya kati, katika wakati ambapo ulimwengu umeelekeza macho yake katika moto unaoteketeza msitu wa mvua wa Amazon huko Brazil.
Msitu wa Bonde la Kongo - sehemu inayofunika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Gabon, Kongo-Brazzaville na Cameroon - unashika nafasi ya pili duniani baada ya msitu wa Amazon na unajulikana kama 'pafu la pili la kijani la dunia.
Shirika hilo limesema tangu Agosti 21, kumeshuhudiwa moto zaidi ya mara 6,902 nchini Angola na mara 3,395 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mara nyingi katika eneo la savanna.
Wataalam wanasema moto katika msitu wa Amazon unatokana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na ukame, wakati moto wa msitu wa Afrika ya kati mara nyingi huwa wa msimu na husababishwa na njia za kilimo za kukata na kuchoma miti.