1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Grossi aonya kuhusu mapigano karibu na kinu cha Kursk

27 Agosti 2024

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Kudhibiti Matumizi ya Nishati ya Atomiki – IAEA Rafael Grossi ameonya kuwa mapigano yanayoendelea karibu na kinu cha nyuklia cha Kursk nchini Urusi yanasababisha hatari kubwa.

Mkuu wa IAEA Rafael Grossi
Rafael Grossi amefanya ziara katika kinu cha Kursk nchini Urusi na kujionea hali ilivyo kutokana na mapiganoPicha: Matthias Schrader/AP Photo/picture alliance

Hayo ni wakati Ukraine ikisema kuwa askari wake wamekamata udhibiti wa kubwa la mkoa wa Kursk nchini Urusi tangu walipofanya uvamizi wa kushtukiza wiki tatu zilizopita. 

Akizungumza wakati wa ziara yake katika kinu cha nyuklia cha Kursk nchini Urusi, Grossi amesema ziara yake imemwezesha kuchunguza sehemu muhimu za kiwanda hicho, ambacho kiko umbali wa chini ya kilomita 50 kutoka uwanja wa mapambano kati ya vikosi vya Urusi na Ukraine. "Tunaona kiwanda bado kinafanya kazi. Lakini wakati huo huo, ukweli kwamba kinafanya kazi ni hatari zaidi kama kutafanywa shambulizi lolote hapo. Wakati kiwanda hicho kinafanya kazi, joto linakuwa juu zaidi. Na kama kutakuwa na mripuko wowote au kitu kinachoweza kukiathiri, kutakuwa na madhara makubwa mno"

Grossi amesema anawasiliana kwa karibu na maafisa wa Urusi na ataziru Kyiv wiki ijayo ili kuzungumza na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, akiongeza kuwa ni muhimu kuzungumza na kuendeleza mazungumzo.

Vikosi vya Ukraine vimeendelea kusonga ndani ya mkoa wa Kursk nchini UrusiPicha: Chubotin Kirill/Ukrinform/ABACA/IMAGO

IAEA imeonya mara kwa mara kuhusu hatari ya kufanyika mapigano karibu na vinu vya nyuklia kufuatia uvamizi kamili wa jeshi la Urusi nchini Ukraine Februari 2022.

Soma pia: Urusi yashambulia miundombinu ya nishati ya Ukraine

Katika siku za mwanzo za mzozo huo, vikosi vya Urusi vilikikamata kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia kusini mwa Ukraine, na pia kikakishikilia kwa muda kiwanda kilichosimamishwa kazi cha Chernobyl katika upande wa kaskazini.

Zelensky amesema leo mjini Kyiv kuwa vita hivyo hatimaye vitamalizwa kwa mazungumzo, lakini Kyiv inapaswa kuwa katika nafasi nzuri na kwamba atawasilisha mpango wa kufanikisha hilo kwa Rais wa Marekani Joe Biden na viongozi wawili wanaotarajiwa kumrithi.

Ukraine yakamata sehemu kubwa ya Kursk

Kwenye uwanja wa mapambano, mkuu wa majeshi ya Ukraine Jenerali Oleksander Syrskyi amesema askari wa nchi hiyo wamekamata udhibiti wa karibu kilomita 1,300 za mraba za eneo la Kursk nchini Urusi tangu uvamizi wao wa kushtukiza wiki tatu zilizopita.

Jenerali Syrstyi pia amesema Ukraine imewakamata wafungwa 600 wa Urusi katika operesheni yake. "Kwa kweli, operesheni ya Kursk ilibadilisha idadi kubwa ya vikosi vyake. Kufikia sasa, tunaweza kusema kwamba karibu wanajeshi 30,000 wametumwa Kursk na idadi hii inaongezeka. Hii inamaanisha kuwa adui anajaribu kuhamisha vikosi kutoka kwa maeneo mengine ya mapambano. Hata hivyo, huko Pokrovsk, Urusi wanafanya kinyume, wanaongeza juhudi zao."

Ujerumani: Hatutaiacha Ukraine kwenye vita peke yake

02:23

This browser does not support the video element.

Madai ya mkuu wa majeshi, ambayo hayajathibitishwa na vyanzo huru, yamejiri saa chache baada ya Ukraine kukabiliwa na wimbi la mashambulizi ya makombora ya Urusi ya kutokea angani kwa usiku wa pili mfululizo.

Watu watano waliripotiwa kufa na wengine 16 wakajeruhiwa katika mashambulizi hayo, ambayo Rais Volodymyr Zelensky amesema yalijumuisha droni 81, Pamoja na makombora ya masafa marefu.

Operesheni ya Kursk, ambayo ndio uvamizi mkubwa zaidi nchini Urusi tangu Vita Vikuu Vya Pili vya Dunia, imewalazimu wakaazi 130,000 kuhama makaazi yao.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema leo kuwa Ukraine imepata hasara kubwa katika mkoa wa Kursk, ambapo karibu askari 6,600 wameuawa au kujeruhiwa  na zaidi ya vifaru 70 vimeharibiwa Pamoja na magari ya kijeshi. Takwimu hizo hazijathibitishwa na vyanzo huru.