1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GSU Kenya washitakiwa mauaji ya mwandishi wa Kipakistani

31 Oktoba 2023

Kitengo maalum cha polisi nchini Kenya, GSU, kimefunguliwa rasmi mashitaka kwa mauaji ya mwandishi habari na mkosoaji wa Kipakistan yaliyotokea Nairobi mwaka mmoja uliopita.

Mwadishi wa habari wa Pakistan aliyeuawa nchini Kenya mwezi Oktoba 2022, Arshad Sharif.
Mwadishi wa habari wa Pakistan aliyeuawa nchini Kenya mwezi Oktoba 2022, Arshad Sharif.Picha: AAMIR QURESHI/AFP/Getty Images

Kesi hiyo ilifunguliwa kwa pamoja baina ya aliyekuwa mke wa mwandishi huyo na vyama viwili vya waandishi habari nchini Kenya.

Arshad Sharif aliuawa tarehe 23 Oktoba 2022, wakati gari aliyokuwamo yeye na raia mwenzake wa Pakistan ilipokwepa kizuizi cha polisi nje ya mji mkuu, Nairobi, na polisi kuifyatulia risasi.

Soma zaidi: Mwandishi wa habari maarufu wa Pakistani auawa nchini Kenya

Polisi ya Nairobi kwa wakati huo ilielezea kujutia tukio hilo, ikisema yalikuwa mauaji ya kimakosa kwa sababu walikuwa wakisaka gari sawa na hilo lililokuwa limehusika na kisa cha utekaji nyara wa mtoto.

Lakini timu ya wapelelezi kutoka Pakistan walisema mauaji ya Sharif yalikuwa ya kupangwa. 

Mwanahabari huyo aliyekuwa na umri wa miaka 50 alikuwa ameikimbia Pakistan mapema mwaka huo ili kuepuka kukamatwa nyumbani kwa mashitaka ya kuzidhalilisha taasisi za dola.