1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guaido aliomba jeshi kususia uchaguzi Venezuela

8 Septemba 2020

Kiongozi wa upinzani Venezuela Juan Guaido amelitaka jeshi la nchi hiyo kuunga mkono hatua ya kususia uchaguzi wa bunge unaopangwa Desemba na kusaidia kuongeza shinikizo la kimataifa dhidi ya Rais Nicolas Maduro. 

Venezuela Caracas | Wahlboykott | Oppositionsführer Juan Guaido
Picha: Getty Images/E. Gamez

Katika hotuba aliyorusha kwenye mitandao ya kijamii, Guaido ameuomba uongozi wa kijeshi kujiunga katika kile alichokiita "muafaka wa umoja” wa nguvu za upinzani kuzuia kuandaliwa kwa uchaguzi wa Desemba 6. Guaido amewaambia wanajeshi kuwacha kujificha katika sketi za kiongozi ambaye ni dikteta na kukoma kupuuza ukweli wa mambo nchini Venezuela. Jeshi linaonekana kuwa nguzo muhimu ya utawala wa Maduro, pamoja na washirika wake Urusi na Iran.

Guaido na viongozi wakuu wa upinzani wameapa kususia uchaguzi wa Desemba 6 kuhusiana na ukosefu wa uwazi baada ya Mahakama ya Juu inayomuunga mkono Maduro kuwateuwa maafisa wa uchaguzi – jukumu ambalo lingestahili kufanywa na bunge ambalo linadhibitiwa na wajumbe wengi wa upinzani.

Karibu vyama 37 vya upinzani vinaunga mkono kususia uchaguzi na kile kinachofahamika kama muafaka wa "kuongeza shinikizo la kimataifa dhidi ya udikteta,” kwa mujibu wa Guaido.

Kiongozi wa upinzani Venezuela Henrique CaprilesPicha: picture-alliance/AP Photo/F. Llano

Hata hivyo, baadhi ya vigogo wa upinzani, wamezungumza wazi kuunga mkono kushiriki katika uchaguzi huo, akiwemo Henrique Capriles, kiongozi anayeheshimika sana ambaye amewahi kugombea urais mara mbili

Mbunge mwingine maarufu wa upinzani, Stalin Gonzalez, pia alijitenga waziwazi wiki iliyopita na kundi linalounga mkono kususia uchaguzi, akisema kuwa kuuhamasisha upinzani katika uchaguzi ni bora zaidi kuliko kususia.

Serikali ya kisoshalisti ya Maduro inalengwa na mfululizo wa vikwazo vya kimataifa, vikiwemo vikwazo vya biashara ya mafuta nchini Marekani, na yeye na washirika wake wa karibu wameshitakiwa kwa ulanguzi wa dawa za kulevya na Wizara ya Sheria ya Marekani.

Mnamo Januari 2019, spika wa bunge la taifa Guan Guiado aliupinga uongozi wa Maduro kwa kujitangaza kuwa kaimu rais, akidai kuwa Maduro aliiba kura katika uchaguzi uliokumbwa na udanganyifu wa 2018 ambao aliibuka mshindi.

Tangu wakati huo, upinzani umejaribu bila mafanikio kumuondoa Maduro, ikiwa ni pamoja na uvuguvugu la uasi wa kijeshi lililoshindwa Aprili 2019 ambalo liliandaliwa na Guaido na ambalo halikupata uungwaji mkono wa kutosha.

Mwandishi: Bruce Amani
afp