Guaido azidi kumuwekea mbinyo Maduro kupitia misaada
21 Februari 2019Hali hiyo inaongeza wasi wasi juu ya makabiliano makubwa mwishoni mwa juma, kati ya rais Maduro na Guaido.
Guaido, ambaye ameweka siku ya mwisho ya Jumamosi kuweka kuingiza misaada, amepanga kuondoka mapema asubuhi leo Alhamis katika msafara wa mabasi pamoja na wajumbe wa bunge la taifa linalodhibitiwa na upinzani, kulazimisha makabiliano makubwa na rais Nicolas Maduro.
Kwa amri ya Maduro, jeshi limeongeza ulinzi mpakani na kuweka vizuwizi katika daraja muhimu la mpakani kuzuwia biadhaa hizo kuingia katika nchi yake kutoka Cucuta, Colombia, ambako tani kadhaa za mahitaji zimelundikana.
Licha ya kwamba hakuna hakika hasa kile ambacho Guaido anataka kufanya , amesema ameorodhesha mamia kwa maelfu ya watu wa kujitolea katika siku za hivi karibuni kusaidia kuleta biadhaa hizo pamoja na kuzigawa.
Jana Jumatano , aliwahamasisha madereva wa mabasi kwenda katika mpaka na kubeba bidhaa hizo za msaada kwa ajili ya Wavenezuela wanaotaabika kutokana na upungufu wa bidhaa hizo.
Hatuogopi
"Hata kama watatuelekezea bunduki , na sisi wote tumepokea vitisho, risasi za mipira na hata risasi za moto , hatuogopi," Guaido alisema, akiwa amesimama juu ya lori akizungukwa na maelfu ya waungaji wake mkono.
"Tutasimama mitaani vifua wazi , tukidai uhuru kwa Wavenezuela wote."
Shehena ya chakula na madawa kwa ajili ya watu waliokumbwa na mzozo imekuwa lengo kuu la mvutano wa madaraka kati ya Maduro na Guaido.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 35 wa bunge la Venezuela alijitangaza kuwa kaimu rais Januari 23, na tangu wakati huo amepata uungwaji mkono wa zaidi ya nchi 50.
Anataka kumuondoa madarakani Maduro, kuunda serikali ya mpito na kufanya uchaguzi. "Hii inaweza kufikiwa hivi karibuni, kati ya miezi sita na tisa, mra pale upinzani wa Maduro utakapomalizika," Guaido ameiambia televisheni ya Mexico Televisa.
Guaido ambaye anasema watu zaidi ya laki tatu huenda wakafariki iwapo misaada hiyo haitaingia, amesema ana lengo la kuwataka mamilioni ya watu wa kujitolea kuanza kuingiza msaada huo nchini humo ifikapo Jumamosi.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Yusuf Saumu