1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guerreiro atangaza kuondoka Borussia Dortmund

29 Mei 2023

Beki shoto raia wa Ureno Raphaël Guerreiro ametangaza kuondoka Borussia Dortmund jana Jumapili, siku moja tu baada ya klabu hiyo kupoteza ubingwa wa Bundesliga kwa Bayern Munich.

FC Chelsea - Borussia Dortmund
Picha: David Inderlied/dpa/picture alliance

Kupitia akaunti yake ya mtandao wa Twitter, Guerreiro amewaandikia mashabiki wa Dortmund kwamba baada ya miaka saba ya kuichezea klabu hiyo, ni wakati wa kuiaga japo kwa huzuni. Beki huyo ameongeza kuwa, kumbukumbu alizozipata akiwa Dortmund zimemfundisha mambo mengi na kumkuza kama mchezaji.

Guerreiro alicheza kama kiungo na kufunga bao katika sare ya 2-2 na Mainz katika mechi ya mwisho ya Bundesliga Jumamosi iliyopita.

Matokeo hayo hayakuwa mazuri kwani Dortmund ilipoteza ubingwa kutokana na tofauti ya wingi wa mabao.

Ujumbe wake wa Instagram ulijumuisha picha akionekena mwingi wa huzuni kufuatia kipenga cha mwisho katika pambano dhidi ya Mainz.

Guerreiro mwenye umri wa miaka 29 ameichezea Dortmund mechi 36 msimu huu, huku akifanikiwa kufunga mabao 6 na kutoa pasi 14 za kuzalisha mabao, lakini amekataa ofa ya kuichezea klabu hiyo kwa miaka miwili mingine.

Raphael Guerreiro akisherehekea baada ya kuifungia bao timu yake ya taifa Ureno wakati wa michuano ya Kombe la Dunia nchini Qatar.Picha: Harry Langer/DeFodi Images/picture alliance

"Sitosahau mapenzi niliyopata kutoka kwa mashabiki na wachezaji wenzangu katika miaka saba ya kuichezea Borussia Dortmund," ameandika Guerreiro ambaye pia alishinda Kombe la Shirikisho la Ujerumani la DFB-Pokal mara mbili na Dortmund.

Ameeleza kuwa, kuiaga klabu hiyo ni kitu kigumu sana katika maisha yake ya soka.

Aliwasili Ujerumani kama kinda wa miaka 22 akitokea Lorient nchini Ufaransa mwaka 2016, na kwa ujumla ameifungia Dortmund mabao 30 katika mechi 162 za Bundesliga.

Hakueleza anaelekea klabu gani japo tetesi zinasema kuwa Atletico Madrid na klabu kadhaa za Uingereza zinafukuzia saini yake.

Katika ngazi ya kitaifa, ameichezea Ureno mechi 62 na kuisaidia timu hiyo kushinda taji la michuano ya Ulaya mnamo mwaka 2016.

Kwa sasa hivi, Dortmund inaripotiwa kufanya mazungumzo na beki shoto wa Algeria Ramy Bensebaini ili kuchukua nafasi yake. Mkataba wa Bensebaini anayechezea klabu ya Borussia Mönchengladbach unakamilika mwishoni mwa msimu.

Dortmund pia huenda ikazikosa huduma za Jude Bellingham na Mahmoud Dahoud ambao wote wanatarajiwa kuondoka.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW