1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guinea: Usalama waimarishwa mjini Conakry baada ya shambulizi dhidi ya Camara

Nina Markgraf4 Desemba 2009

Serikali ya kijeshi nchini Guinea imeimarisha usalama katika mji mkuu, Conakry, siku moja baada ya kiongozi wa kijeshi, nchini humo, Kapteni Camara kupigwa risasi.

Kapteni Moussa Dadis Camara ajeruhiwa, katikma shambulio lililotekelezwa na wanajeshi wake.Picha: dpa

Kapteni Moussa Dadis Camara alijeruhiwa kufuatia jaribio la kutaka kumuua lililofanywa na wanajeshi wake.

Hakuna taarifa zozote kuhusiana na iwapo, Aboubakar Toumba Diakite, anayetuhumiwa kuhusika na shambulizi hilo amekamatwa. Diakite alikuwa mlinzi wa zamani wa Camara.

Kapteni Camara anatibiwa katika makao makuu ya kijeshi, baada ya kukataa msaada wa Senegal iliyotuma ndege kumsafirisha kiongozi huyo wa kijeshi mjini Dakar kwa matibabu.

Raia wa Guinea waangalia maiti za watu waliouawa na wanajeshi, katika maandamano, mnamo Septemba.Picha: DPA

Ni tukio lililowashtua raia wengi nchini Guinea, na hasa katika mji mkuu wa Conakry. Inaripotiwa kwamba ufyatulianaji wa risasi ulianza muda mfupi baada ya kiongozi wa kijeshi Kapteni Moussa Dadis Camarra alipokuwa anazuru kambi moja ya kijeshi, jana jioni.

Camarra alijeruhiwa, katika shambulizi hilo. Walioshuhudia kisa hicho wanasema kulitokea hali ya wasiwasi pale, wanajeshi kutoka kambi nyingine ya kijeshi walipomiminika kati kati mwa mji wa Conakry, wakiwa wanawasaka washukiwa waliotekeleza shambulizi hilo dhidi ya Camarra.

Waziri wa habari Idrissa Cherif alitoa taarifa fupi akisema Kapteni Mouusa Dadis Camara alijeruhiwa, lakini hali yake haiko hatarini na kwamba anapata matibabu katika makao makuu ya kijeshi.

Muda mfupi tu baada ya shambulizi hilo, nchi jirani ya Senegal ilituma ndege na madaktari, kumsafirisha Camara hadi mjini Dakar iwapo alihitaji matibabu ya ziada.

Afisa wa serikali hiyo ya kijeshi lakini alisema majeraha aliyoyapata Camara si makubwa mno, na kwamba atatibiwa tu katika makao makuu ya kijeshi.

Hakuna taarifa zozote kuhusiana na iwapo Abobakar Toumba Diakite, amekamatwa. Diakite ambaye alikuwa mlinzi wa zamani wa Camarra anatuhumiwa kuwa mhusika mkuu wa shambulizi hilo dhidi ya Kapteni Camara. Diakite pia anatuhumiwa kuwa ndiye aliyeongoza yale mauaji ya watu 150, pale wanajeshi walipowavamia watu katika uwanja wa michezo kwa mkutano wa upinzani, na kuwamiminia risasi, mnamo mwezi Septemba.

Kapteni Captain Moussa Dadis Camara, akitembea na waziri mkuu Kabine Komara.Picha: DPA

Shambulizi la jana dhidi ya Camarra lilitokea wakati wachunguzi kutoka Umoja wa Mataifa walipokuwa wanamalizia ucghunguzi wake kuhusiana na mauaji hayo yaliyotekelezwa na wanajeshi. Mashirika ya haki za kibinadamu yanasemekana yamemtaja Diakite kama mhusika mkuu katika mauaji hayo ya raia 150 waliokuwa wanapinga Kapteni Camara asiwe mgombea katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani. Viongozi wa kijeshi nchini Guinea huenda wakafunguliwa mashtaka na mahakama ya kimataifa kuhusiana na mauaji hayo.

Kulingana na mwanadiplomasia mmoja, jaribio la mauaji dhidi ya Camarra lina uhusiano mkubwa na uchunguzi huo wa Umoja wa Mataifa. Kulingana na mwanadiplomasia huyo, Camara, anajaribu kuweka lawama zote za mauaji ya septemba katika mabega ya Diakite, ili ajiondolee lawama yeye mwenyewe. Kapteni Moussa Dadis Camarr alichukua mamlaka ya uongozi muda mfupi tu baada ya kufariki kwa rais Lansana Conte, Desemba mwaka uliopita. Camara alikuwa ameahidi atapena madaraka, lakini hadi sasa amekatalia uongozini.

Mwandishi: Munira Muhammad/ AFPE

Mhariri: Aboubakary Liongo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW