1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guinea -watu 157 wauwawa

30 Septemba 2009

Guinea yaomboleza siku 2 za huzuni.

Captain Moussa Daddis Camara.Picha: dpa

Jamhuri ya Guinea huko Afrika ya magharibi,imepiga leo marufuku mkusanyiko wowote wa kichochezi na imetangaza siku 2 za maombolezi baada ya wanajeshi kuwafyatulia risasi na kuwaua si chini ya waandamanaji 157 na kuwajeruhi wengine 1.253 kufuatia mkomoto dhidi ya maandamano ya wafuasi wa upinzani.

Mtawala wa kijeshi wa Mali ,Captaini Moussa Dadis Camara, amesema anasikitishwa na machafuko yaliozuka .Chama kinachotetea haki za binadamu lakini, kimesema kwamba, wanajeshi wamewaua watu 3 zaidi nje ya mji mkuu wa Guinea-Conackry hii leo.

"Ninatangaza maombolezi kwa Taifa zima hii leo na kesho.Mkusanyiko wowote wa kundi la watu wenye shabaha ya kufanya uchochezi ni marufuku."

Kiongozi wa utawala wa kijeshi wa Guinea, Capteni Moussa Camara , alinadi kwenye TV -siku moja baada ya jeshi lake kuwafyatulia risasi waandamanaji wa Upinzani na kuwanyakua wahanga kutoka mahospitali walikokimbilia kwa matibabu.

Mtawala huyo wa kijeshi Moussa camara akawataka masheikh wa kiislamu na makasisi wa kikristu nchini ,viongozi wa kisiasa na wa kiraia na hata waandishi habari kujizuwia n a vitendo vinavyoweza kuchafua usalama nchini.Akaomba ibada maalumu ya kitaifa ijumaa na Jumapili hii ijayo ili kuwakumbuka waliopoteza maisha.

Wakereketwa wa haki za binadamu nchini Guinea, wanadai kwamba, watu 3 zaidi wameuliwa leo ."Vijana walitoka nje na wanajeshi wakawafyatulia risasi." Afisa wa chama cha Haki za binadamu cha Guinea, Maadjou Sow alisema zaidi kwamba, wanajeshi waliwanyakua majeruhi kutoka mahospitali na kuwapeleka sehemu zisizojulikana.

Ufaransa, mkoloni wa zamani wa Jamhuri ya Guinea, imetangaza kusimamisha misaada yote ya kijeshi na Guinea pamoja na kuudurusu uhusiano wake na nchi hiyo.Umoja wa Mataifa,Umoja wa Afrika na hata Umoja wa Ulaya ,Marekani na Kanada , zote zimeelezea kustushwa kwao na mauaji ya juzi Jumatatu katika Uwanja wa mpira ambako maalfu ya wapinzani wa serikali, walihudhuria mkutano kumpiga Kepteni Moussa Camara. Wapinzani hao wakipinga jaribio lolote la mwanajeshi huyo kuania urais katika uchaguzi ujao Januari,mwakani.

Kapteni Moussa Camara , anashinikizwa mno na Jamii ya kimataifa kuacha madaraka. Alinyakua madaraka baada ya kuongoza njama ya mapinduzi yasio-mwaya damu masaa tu baada ya Kiongozi wa Guinea,marehemu Lansana Conte, alietawala Guinea tangu 1984, kuaga dunia.Upinzani nchini Guinea, unautuhumu utawala wa kijeshi kuwaua hadi watu 157 na kuwajeruhi wengine 1.253.

Mamadi Kaba ,mkuu wa tawi la Afrika la chama cha haki za binadamu nchini Guinea (RADDHO), amesema kuwa, ubakaji wa wanawake ulianzia huko huko Uwanja wa mpira.Akasema zaidi kwamba, wanajeshi waliwabaka akina mama uwanjani na kuendelea kufanya hivyo katika kambi zao za kijeshi.

Muandishi: Ramadhan Ali /AFPE

Mhariri: O.Miraji

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW