Guinea ya Ikweta na Libya kufungua dimba kombe la Afrika
21 Januari 2012Tamasha kama hili kubwa la michezo linalofanyika kila baada ya miaka miwili haliwezi kukamilika , hata hivyo , bila kuwa na aina yake ya utata, na tamasha la mwaka huu halina tofauti.
Mara hii wakati wa kuelekea kuanza kwa tamasha hilo mjini Bata ambako Guinea ya Ikweta inakumbana na Libya katika mchezo wa ufunguzi kumekuwa na malalamiko kutoka Burkina Faso na Zambia kuhusiana na malazi huku timu zote zililazimika kubadilisha hoteli walizopangiwa.
Tulipowasili hapa , walituweka katika mgahawa . Ilikuwa hata haina hadhi ya hoteli. Hakuna chumba cha video, hakua chumba cha mikutano. Kila mara inabidi kufanya ujanja tu. Hivi ndivyo kombe la Afrika linavyokuwa, amelalamika kocha wa Burkina Faso Paulo Duarte.
Nadhani watu wanapaswa kuwa na heshima na timu ya taifa ya Zambia. Sio mara yetu ya kwanza kufikia katika fainali hizi, ameongeza kocha wa Zambia Herve Renard
Watayarishaji wa mashindano hayo ya CAF wamejibu kwa kusema kuwa hoteli ambazo timu zimepangiwa zimechaguliwa kutokana na kura, ili kuepuka kutowatendea haki timu yoyote.
Kama chakula maalum kilichoandaliwa bila ya kuwa na mgeni maalum tamasha hili la soka linafanyika bila ya kuwapo mabingwa mara tatu wa fainali tatu zilizopita Misri.
Mbali na Misri vigogo wengine katika soka la Afrika , Cameroon , Nigeria, Algeria na Afrika kusini pia wameshindwa kufuzu kuingia katika fainali za mwaka huu.
Katika timu hizi nne vigogo vya soka , Ghana ambayo imefikia robo fainali ya kombe la dunia na Cote D'Ivoire ya Didier Drogba ni timu zinazoonekana kuwa na uwezo wa kutoroka na kombe hilo, ambalo limewapiga chenga kwa muda mrefu.
Orodha ya timu zilizoingia fainali ya mwaka huu katika kombe la Afrika inamaajabu yake, mojawapo ni Libya ambayo imefanikiwa kufuzu kuingia katika fainali hizi mbali ya matatizo ya kisiasa na vita nchini mwake , hali iliyosababisa kuondolewa madarakani kwa kiongozi wa muda mrefu wa nchi hiyo Mouammar Gaddafi na hatimaye kuuwawa.
Heko pia ziwaendee Niger na Botswana , timu hizi mbili ambazo zinaonekana kuwa ni wanagenzi pamoja na Guinea ya Ikweta ambayo imeingia katika kinyang'anyiro hicho kutokana na kuwa mwenyeji mwenza wa mashindano hayo wamejiweka katika meza kuu ya soka la Afrika kwa sasa.
Hata hivyo vyota wa soka wa zamani katika bara la Afrika wameonya zile ztimu ambazo zinaonekana kuwa na uwezo wa kulinyakua kombe hilo kuwa makini na timu zinazoonekana kuwa dhaifu kama Botswana na Niger wakati muda unakaribia wa kuanza kwa mashindano hayo. Abedi Pele, Ayew wa Ghana , Rogobert Song wa Cameroon na Mustapha Hadji wa Morocco wamekubali kuwa maelezo kuwa Cote D'Ivoire na Ghana zitafikia fainali hapo tarehe 12 February ni mapema mno na kwamba kunaweza kutokea maajabu kabla ya vumbi kutua katika viwanja hivyo nchini Guinea ya Ikweta na Gabon.
Mwandishi : Sekione Kitojo / AFPE
Mhariri : Sudi Menette